KAMATI YA MIPANGO NA FEDHA YABAINI CHANGAMOTO YA UKUSANYAJI MAPATO, YATOA MAPENDEKEZO YA KUBORESHA UFANISI
Na Joseph Ngilisho|LONGIDO
Kamati ya Mipango na Fedha ya halmashauri imebaini kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazoathiri mwenendo wa ukusanyaji wa mapato, huku baadhi ya vyanzo vikishindwa kufikia malengo yaliyowekwa.
Akisoma taarifa ya kamati hiyo katika kikao cha baraza la madiwani, Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Fedha, Peter Lekaneth alisema pamoja na jitihada zinazofanywa na menejimenti ya halmashauri, bado kumekuwa na mwenendo usioridhisha wa ukusanyaji wa mapato hususan katika maeneo ya ada ya ukaguzi wa nyama, ada za machinjio, ushuru wa minada, magulio pamoja na ushuru wa mazao.
Alisema kamati imeendelea kutumia njia mbalimbali katika kusimamia utekelezaji wa majukumu yake, ikiwemo kufanya uchambuzi wa mapato na matumizi ya halmashauri kwa kipindi cha Januari hadi Machi pamoja na kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji kutoka idara na vitengo mbalimbali.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, halmashauri ilikuwa imekadiria kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 5.8 za mapato ya ndani, lakini hadi mwezi Machi ilikuwa imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 3.4 sawa na asilimia 67 ya makisio ya mwaka.
Aidha, matumizi ya fedha hadi kipindi hicho yalikuwa yamefikia asilimia 58 ya fedha zilizokusanywa.
Kamati pia ilieleza kuwa halmashauri imeendelea kufanya jitihada za kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato kwa kupanga kufanya kikao na wafanyabiashara pamoja na wafugaji ili kuwapa elimu kuhusu umuhimu wa kuchangia mapato ya halmashauri kupitia ushuru mbalimbali katika minada na maeneo mengine ya biashara.
Katika hatua nyingine, kamati ilisema halmashauri imeendelea kufuatilia suala la kuachiwa baadhi ya masoko ya awali, ambapo viongozi wa halmashauri walifika wizara husika kwa ajili ya kulipigania jambo hilo.
Kutokana na changamoto zilizobainika, kamati ilitoa mapendekezo mbalimbali kwa menejimenti ya halmashauri ikiwemo kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato, kufanya tathmini ya vyanzo vinavyofanya vibaya, kuweka malengo ya kila siku, wiki na mwezi kwa wakusanyaji pamoja na kuimarisha ukaguzi wa ndani.
Mapendekezo mengine ni kuchukua hatua kwa vyanzo vinavyokusanya chini ya asilimia 10 au sifuri, kufanya tathmini ya vyanzo vinavyofanya vizuri ili kuongeza makusanyo pamoja na kufanya vikao vya tathmini kila mwezi ili kubaini mapungufu mapema.
Kamati pia ilisisitiza kuwa matumizi yote ya fedha za halmashauri nje ya bajeti yaliyoidhinishwa lazima yapate ridhaa ya kamati kwa mujibu wa taratibu za serikali.
Katika eneo la maendeleo, kamati ilieleza kuwa utekelezaji wa miradi mbalimbali unaendelea vizuri huku miradi 39 ikitajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kukamilika ndani ya mwaka wa fedha husika.
Aidha, kamati ilijadili maombi ya mabadiliko ya vifungu vya matumizi katika bajeti ya mwaka 2025/2026 pamoja na utekelezaji wa programu ya kujenga uwezo wa halmashauri katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kamati ilitoa rai kwa mkurugenzi mtendaji kuhakikisha asilimia 20 ya mapato ya ndani yanatolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama ilivyopangwa kwenye bajeti ya halmashauri.
Pia vijiji na wadau wote walitakiwa kutoa ushirikiano wa kutosha katika kusimamia mashauri yaliyopo mahakamani ili kulinda maslahi ya halmashauri.
Ends



0 Comments