DOYO AVITAKA VYAMA VYA SIASA KUHESHIMU SHERIA, APONGEZA HATUA ZA MSAJILI
Na Hadija Bagasha, Tanga
Aliyekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, amevitaka vyama vya siasa nchini kuachana na siasa za mihemko na badala yake kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zinazosimamia usajili na uendeshaji wa vyama vya siasa ili kulinda amani na utulivu wa taifa.
Doyo, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, alisema hatua ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuiandikia barua Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuomba ufafanuzi kuhusu kauli ya mmoja wa viongozi wake ni ishara kuwa sheria inasimamiwa kwa usawa kwa vyama vyote vya siasa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga kuhusu mwenendo wa siasa nchini, Doyo alisema hatua hiyo imeongeza matumaini kwa wananchi na wadau wa siasa kwamba hakuna chama kitakachopewa upendeleo mbele ya sheria.
Alisisitiza kuwa hakuna chama, mwanasiasa wala mwanaharakati anayepaswa kujiona yupo juu ya sheria, huku akiitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuendelea kusimamia sheria bila woga wala upendeleo.
“Kuna wanaharakati na wanasiasa wanaojiona wapo juu ya sheria na wanaweza kusema chochote huku wakitishia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, wakisahau kuwa ofisi hiyo ipo kisheria na ina mamlaka kamili,” alisema Doyo.
Aidha, aliitaka ofisi hiyo kuendelea kuchukua hatua dhidi ya vyama au viongozi watakaobainika kwenda kinyume na sheria bila kuangalia ukubwa wa chama au ushawishi wake wa kisiasa.
Kwa mujibu wa Doyo, taasisi yoyote inayosimamia sheria inaposhindwa kutekeleza wajibu wake kwa wakati hujenga mazingira ya sintofahamu, migogoro na kudhoofika kwa nidhamu ya kisiasa nchini.
“Tutakapokuwa na taasisi isiyo na uwezo wa kushughulikia changamoto za eneo inalolisimamia, matokeo yake ni migogoro na uvunjifu wa amani. Ndiyo maana tumeamua kuzungumza mbele ya Watanzania ili kusisitiza kuwa kila upande unapaswa kuwajibika kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Katika hatua nyingine, Doyo aliipongeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kile alichodai kuwa ni uthubutu wa kuchukua hatua kwa vyama mbalimbali vya siasa bila upendeleo.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alisema pamoja na kuwepo kwa mjadala mkubwa wa kisiasa, chama hicho kilitoa majibu kwa Msajili kama ilivyotakiwa kisheria.
“Msajili aliwaandikia barua CHADEMA na mwisho wa siku wakatoa majibu yao. Hii inaonyesha kuwa sheria lazima ifuatwe,” alisema.
Doyo alisema hatua ya Msajili kuiandikia barua CCM pia imeonyesha wazi kuwa sheria haifanyi kazi kwa upande mmoja pekee, bali kwa vyama vyote bila ubaguzi.
“Tumeona Msajili amekichukulia hatua pia Chama Cha Mapinduzi kwa kukiandikia barua ili nao watoe maelezo kuhusu kauli za viongozi wao. Hii inaongeza matumaini makubwa kwa vyama vya siasa pamoja na wananchi kwa ujumla,” alisema.
Aliongeza kuwa ana matumaini CCM nayo itawasilisha majibu yake kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, huku akiendelea kuipongeza ofisi hiyo kwa kutokuyumba katika utekelezaji wa sheria.
“Watu walidhani sheria inafanya kazi kwa upande mmoja, lakini sasa imeonekana wazi kuwa anayevunja sheria ndiye anayechukuliwa hatua bila kujali anatoka chama gani,” alisisitiza Doyo.

0 Comments