MSIGWA WA CCM AREJEA CHADEMA, AITUPIA CCM DONGO ZITO LA UKIUKWAJI WA HAKI

 MSIGWA AREJEA CHADEMA, AITUPIA CCM LAWAMA ZA UKIUKWAJI WA HAKI

Na Joseph Ngilisho – Arusha Digital

ALIYE Mbunge wa Iringa Mjini na kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Peter Msigwa, ametangaza rasmi kurejea katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kusema amefuata taratibu zote zinazotakiwa ndani ya chama hicho.

Mch. Msigwa alitangaza uamuzi huo leo kupitia ukurasa wake wa Instagram, huku akithibitisha pia kupitia mahojiano na Ayotv kuwa taarifa hiyo ni ya kwake binafsi na imechochewa na tafakuri ya kina kuhusu kile alichokiita ukiukwaji wa haki, utu na dhuluma dhidi ya uhai wa binadamu uliojitokeza Oktoba 29, 2025.

Katika ujumbe wake, Msigwa amesema kuwa ameamua kujiondoa rasmi ndani ya CCM na kurejea CHADEMA kutokana na dhamira yake kusimama upande anaouamini kuwa wa kweli na wenye kutetea haki za wananchi.

“Kwa dhamira yangu binafsi leo nimejiondoa rasmi kutoka CCM na kurejea CHADEMA kwa kufuata taratibu zote za CHADEMA, na Watanzania wote pamoja na wanachama wa CHADEMA walioumizwa au kukatishwa tamaa na msimamo wangu wa awali naomba radhi kwa dhati pale nilipokuwa kinyume na matarajio yetu ya pamoja katika safari ya kutafuta haki, utu na demokrasia ya kweli,” amesema Msigwa.

Ameongeza kuwa binadamu hukosea, lakini pale dhamira inapozinduka ni muhimu kusimama katika upande unaotetea ukweli na haki.

“Naam, binadamu hukosea lakini dhamira inapozinduka ni wajibu kusimama upande unaouona kuwa wa kweli na wa haki,” ameongeza.

Hatua ya Msigwa kurejea CHADEMA inatajwa kuwa moja ya matukio makubwa ya kisiasa yanayoweza kuibua mjadala mpya ndani ya siasa za upinzani na CCM, hasa kutokana na historia yake ya kuwa mmoja wa viongozi waliowahi kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya chama hicho pamoja na nafasi yake ya uwakilishi wa wananchi wa Iringa Mjini kwa vipindi tofauti.

Ends

Post a Comment

0 Comments