KAMATI YA MICHEZO ARUSHA YASIKITISHWA NA KIFO CHA MWENYEKITI WA DARTS
Na Joseph Ngilisho – Arusha
KAMATI YA MICHEZO ARUSHA YASIKITISHWA NA KIFO CHA MWENYEKITI WA DARTS MKOA, NAEEM BADRI
Na Joseph Ngilisho – Arusha
Kamati ya Michezo Wilaya ya Arusha imesema imesikitishwa na kifo cha Mwenyekiti wa Chama cha Vishale (Darts) Mkoa wa Arusha, marehemu Naeem Mustapha Badri, aliyefariki dunia leo asubuhi akiwa katika Hospitali ya Mount Meru mjini Arusha.
Taarifa za kifo hicho zimethibitishwa na Katibu wa Darts Mkoa wa Arusha, ambaye amesema mazishi ya marehemu yatafanyika leo saa moja jioni katika makaburi ya Njiro jijini Arusha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na viongozi wa michezo wilayani humo, msiba kwa sasa upo katika Msikiti wa Arusha Art uliopo maeneo ya Posta karibu na duka la Tanga General, ambapo ndugu, jamaa, marafiki pamoja na wadau wa michezo wameendelea kufika kutoa pole kwa familia.
Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Michezo Wilaya ya Arusha, mmoja wa viongozi wa michezo amesema marehemu Naeem Badri alikuwa kiongozi mwenye mchango mkubwa katika kukuza na kuimarisha mchezo wa darts mkoani Arusha na nchini kwa ujumla.
Amesema marehemu alikuwa daraja muhimu kati ya chama cha darts na serikali, huku akitumia nafasi yake kuhamasisha vijana kushiriki michezo pamoja na kuendeleza mshikamano miongoni mwa wanamichezo.
“Tumepokea kwa huzuni kubwa taarifa za kifo cha mwenzetu na kiongozi wetu. Marehemu Naeem Badri alikuwa mtu wa watu, mwenye ushawishi mzuri katika maendeleo ya michezo, hasa darts. Amefanya kazi kubwa kuunganisha wadau wa michezo na taasisi mbalimbali za serikali,” amesema kiongozi huyo.
Aidha, viongozi wa michezo wameeleza kuwa enzi za uhai wake, marehemu alikuwa mstari wa mbele kusimamia mashindano mbalimbali ya darts, kuibua vipaji vya vijana na kuhakikisha mchezo huo unapata nafasi kubwa katika jamii.
Baadhi ya wanamichezo na wadau wa darts waliozungumza kwa nyakati tofauti wameeleza kushtushwa na taarifa za kifo hicho wakisema wamepoteza kiongozi aliyekuwa mwenye maono, mshauri na mlezi wa vijana wengi waliokuwa wakijikita katika mchezo huo.
Wamesema pengo lililoachwa na marehemu litakuwa vigumu kuzibika kutokana na mchango wake mkubwa katika kuendeleza michezo mkoani Arusha.
Kamati ya Michezo Wilaya ya Arusha imeitoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na wanamichezo wote wa darts mkoani humo, huku ikiwataka kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.
**Ends**

0 Comments