ULEGA AANIKA MAPINDUZI YA MIUNDOMBINU ARUSHA, AHAKIKISHA BARABARA ZA KISASA NA MWANGA WA USIKU — AFCON 2027 YAPEWA KIPAUMBELE
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
SERIKALI imezidi kuthibitisha kwa vitendo dhamira yake ya kuimarisha miundombinu ya barabara nchini, baada ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, kuanika kwa kina mafanikio, kasi ya utekelezaji na matarajio ya miradi mikubwa ya barabara jijini Arusha, mbele ya Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa miradi hiyo, Ulega alisema utekelezaji wa barabara hizo ni utekelezaji wa maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, yanayolenga kuboresha miundombinu ili kuchochea ukuaji wa uchumi, kurahisisha usafiri na kuinua ustawi wa wananchi.
Alieleza kuwa miradi hiyo—ikiwemo barabara ya Arusha Bypass pamoja na ile ya Kisongo—inalenga kuimarisha mtandao wa usafiri ndani na nje ya jiji, huku ikifungua fursa mpya za uwekezaji, biashara na ajira kwa wakazi wa mkoa huo na ukanda mzima wa kaskazini.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, maelekezo ya Mheshimiwa Rais yamekuwa dira yetu. Tunajenga barabara hizi kwa viwango vya kisasa ili zidumu na kutoa huduma bora kwa wananchi,” alisisitiza Ulega.
Katika hatua ya kuibadilisha Arusha kuwa jiji la kisasa linalofanya kazi saa 24, Waziri huyo alibainisha kuwa barabara hizo zitakuwa na mfumo mkubwa wa taa za barabarani, ambapo kila kilomita itawekewa wastani wa taa 40. Kwa mujibu wa maelezo yake, barabara ya Arusha Bypass pekee itakuwa na zaidi ya taa 1,600, huku kipande cha kilomita 9 kuelekea Kisongo kikitarajiwa kuwa na zaidi ya taa 550.
Alisisitiza kuwa uwekezaji huo wa mwanga wa barabarani si wa mapambo bali ni nguzo muhimu ya usalama, kupunguza ajali na kuimarisha uchumi wa usiku (night economy), unaotarajiwa kukuza biashara na huduma hata baada ya saa za kazi.
Kwa upande wa utekelezaji, Ulega alisema mkandarasi alianza rasmi kazi Aprili 1, 2026, huku mradi mzima ukitarajiwa kukamilika Aprili 9, 2029. Hata hivyo, alifafanua kuwa Serikali imeelekeza baadhi ya vipande vikamilike mapema ili wananchi waanze kunufaika kabla ya muda wa mwisho.
“Tumesisitiza kasi ya ujenzi iongezwe. Kipande cha kilomita 13 kitakamilika mapema, sambamba na kipaumbele cha kipande cha Mabonde ya Mto hadi Gondeni City chenye kilomita 16,” alieleza.
Akitoa msisitizo wa kisera, Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba alimtaka mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotarajiwa, akisisitiza kuwa miundombinu bora ni uti wa mgongo wa maendeleo ya taifa.
AFCON 2027 YACHOCHEA KASI YA MIRADI
Katika muktadha wa maandalizi ya Africa Cup of Nations 2027, Ulega alisisitiza kuwa Serikali imeweka mkazo maalum kuhakikisha miradi yote ya barabara inayohusiana na mashindano hayo inakamilika kwa wakati.
Alisema maandalizi ya miundombinu ni sehemu ya mkakati mpana wa kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na fursa za kiuchumi, utalii na hadhi ya kimataifa itakayotokana na mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, alisema utekelezaji wa miradi unaendelea kwa mujibu wa ratiba, huku mkandarasi akiwa tayari ameanza kazi katika barabara ya Mbauda–Losinyai na Tanganyika Packers tangu Aprili 10, 2026.
Alifafanua kuwa, licha ya mradi mzima kupangwa kukamilika 2029, kipande muhimu cha kilomita 13 kitakamilika mapema ili kurahisisha usafiri wakati wa AFCON. Kipande hicho kinahusisha Mbauda–Bondeni City (km 9) na Tanganyika Packers–Makutano ya Arusha Bypass (km 4), kikijengwa kwa mfumo wa “Design and Build” ili kuongeza kasi na ufanisi.
Kwa mujibu wa Besta, sehemu ya Mbauda hadi Makutano ya Arusha Bypass (km 7) itajengwa kwa njia nne, huku sehemu ndefu zaidi—ikiwemo Makutano ya Arusha Bypass hadi Losinyai pamoja na Tanganyika Packers hadi Losinyai (km 63)—ikijengwa kwa njia mbili.
Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Company chini ya usimamizi wa Kitengo cha Ushauri wa Kihandisi cha TANROADS (TECU), ambapo hadi sasa mkandarasi amelipwa shilingi bilioni 17.6 kama malipo ya awali.
Sambamba na hilo, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya Soko la Kilombero–Msikiti wa Ngarenaro–Kisongo (km 9.1), ambayo itakuwa na njia nne kuelekea Kisongo na njia mbili upande wa Ngarenaro kuelekea barabara ya Nairobi.
ARUSHA KUWA KITOVU CHA UCHUMI NA UTALII
Uzinduzi wa miradi hiyo unaashiria hatua muhimu katika kuifanya Arusha kuwa kitovu imara cha utalii, biashara na uwekezaji. Miundombinu hiyo inatarajiwa kupunguza gharama za usafirishaji, kuongeza ufanisi wa biashara na kuvutia wawekezaji wapya ndani na nje ya nchi.
Kwa ujumla, miradi hiyo si tu kwamba itaboresha mandhari ya jiji, bali pia itaweka msingi wa mageuzi mapana ya kiuchumi, huku ikiiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kunufaika na matukio makubwa ya kimataifa kama AFCON 2027.
Ends..


0 Comments