WAZIRI APIGA MKWARA MISAFARA MIREFU YA MA-RC,DC NA DED ATAKA WAPANDE BASI
Na Arushadigital| Bahi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, ametoa agizo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kupunguza matumizi ya mafuta kwa kubana misafara ya magari katika ziara za kikazi, akisisitiza utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza Aprili 17, 2026 katika kikao na viongozi wa Mkoa wa Dodoma na Wilaya ya Bahi kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Prof. Shemdoe alisema ni wakati wa viongozi kuonesha uzalendo kwa kutumia rasilimali za umma kwa ufanisi zaidi, hasa katika kipindi ambacho gharama za mafuta zimeongezeka.
Katika kusisitiza hilo, Waziri huyo alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, kwa kuonesha mfano wa kuigwa baada ya kutumia gari moja tu katika ziara yake ya kikazi wilayani Bahi—hatua aliyoitaja kuwa ni utekelezaji halisi wa maelekezo ya Rais.
“Wakuu wa Mikoa na Wilaya muendelee kupunguza misafara yenu mnapokuwa kwenye ziara za kikazi. Kama mlivyoona hivi karibuni, Mheshimiwa Rais ameonesha kwa vitendo. Ni lazima nasi tuige kwa kupunguza matumizi ya mafuta kwa kutumia magari machache iwezekanavyo,” alisisitiza Prof. Shemdoe.
Aliongeza kuwa ana imani viongozi wote wa ngazi za mikoa na wilaya watazingatia agizo hilo, akibainisha kuwa hatua hiyo si tu itapunguza gharama za uendeshaji wa Serikali bali pia itaongeza uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.
Prof. Shemdoe alifafanua kuwa, katika mazingira ya sasa ambapo bei za mafuta zimepanda na kuathiri bajeti za taasisi mbalimbali za Serikali, ni muhimu kwa viongozi kuchukua hatua za haraka kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima, ikiwemo kupunguza idadi ya magari katika misafara yao.
Baada ya kikao hicho, Waziri huyo aliongoza hafla ya kuwapongeza walimu na wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa ya darasa la nne, darasa la saba, kidato cha pili na kidato cha nne.
Hafla hiyo ilifanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Chiona, wilayani Bahi, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na wadau wa elimu.
Kwa ujumla, msisitizo wa TAMISEMI unalenga kuimarisha nidhamu ya matumizi ya rasilimali za Serikali, huku ukihamasisha viongozi kuwa mfano katika kusimamia kwa ufanisi fedha za umma kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

0 Comments