KORONA SEKONDARI YANG’ARA KITAALUMA , SERIKALI YAWEKA MIKAKATI KUTATUA CHANGAMOTO ZILIZOBAINIKA,MAKONDA AOMBWA KUWA MLEZI WA SHULE

 KORONA SEKONDARI YANG’ARA KITAALUMA, SERIKALI YAWEKA MIKAKATI KUTATUA CHANGAMOTO ZILIZOBAINIKA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

SHULE ya Sekondari Korona jijini Arusha imeendelea kuonesha mafanikio makubwa kitaaluma huku serikali ikiahidi kushughulikia changamoto zinazoikabili shule hiyo ili kuimarisha zaidi mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Akizungumza katika Mahafali ya Saba ya Kidato cha Sita yaliyofanyika shuleni hapo April 16 ,2026 ambapo jumla ya wanafunzi 192 walihitimu  na kutunukiwa vyeti, Afisa Elimu Sekondari wa Jiji la Arusha, Mwalimu Joshua Mange, alisema serikali imeanza kuchukua hatua za kushughulikia changamoto mbalimbali zilizobainishwa na wanafunzi pamoja na uongozi wa shule hiyo.

 

Mange alitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na miundombinu duni, upungufu wa walimu katika baadhi ya masomo mapya, huduma za afya kwa wanafunzi pamoja na hali ya barabara inayoelekea shuleni hapo.

“Changamoto hizi si mpya, zimekuwepo kwa muda mrefu. Tumezipokea na tutazifanyia kazi kupitia mifumo rasmi ya serikali ili kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu,” alisema Mange.

Alifafanua kuwa suala la barabara tayari litaingizwa katika vikao vya maendeleo kuanzia ngazi ya kata hadi baraza la madiwani ili lipewe kipaumbele kulingana na upatikanaji wa rasilimali.

Kuhusu upungufu wa walimu, alisema masomo kama Historia, Maadili ya Jamii, Tanzania na Communication Skills yana uhaba wa wataalamu kutokana na maboresho ya mitaala ya hivi karibuni, lakini serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuongeza walimu wenye sifa katika maeneo hayo.

Aidha, alibainisha kuwa tathmini ya mipaka ya shule tayari imefanyika na kubaini haja ya kulipa fidia katika baadhi ya maeneo ili kulinda ardhi ya shule dhidi ya uvamizi, huku hatua za kuingiza suala hilo kwenye bajeti zikiendelea.

Katika kuboresha ustawi wa wanafunzi, Mange alikiri uwepo wa uhitaji wa huduma za afya hasa nyakati za usiku, akiahidi kuwa jitihada zinafanyika kuhakikisha upatikanaji wa mhudumu wa afya au mlezi mwenye ujuzi huo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Korona, Mwalimu Christopher Malamsha, alisema shule hiyo imeendelea kufanya vizuri kitaaluma tangu kuanzishwa kwake, ikiwa na rekodi ya kutokuwa na mwanafunzi aliyewahi kupata daraja la sifuri.

Alisema mahafali hayo ni ya kihistoria kwani yanahusisha kundi la kwanza la wanafunzi walioanza kidato cha tano wakiwa 20 pekee, ambao sasa wanahitimu kwa mafanikio na kujiandaa kujiunga na vyuo vikuu.

“Tunaendelea kujivunia matokeo mazuri kila mwaka. Mwaka jana tulikuwa na watahiniwa 387 ambapo hakuna aliyepata daraja la sifuri, wanafunzi 70 walipata daraja la kwanza na zaidi ya 210 daraja la pili,” alisema Malamsha.

Aliongeza kuwa shule hiyo kwa sasa inatoa tahasusi za PCM na CBG, huku mipango ikiendelea kuongeza PCB na PGM kuanzia Julai mwaka huu ili kupanua fursa kwa wanafunzi.

Katika hatua nyingine, Bodi ya Shule hiyo imemwomba Mbunge wa Arusha Mjini na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kukubali kuwa mlezi wa shule hiyo ili kusaidia kuimarisha maendeleo na nidhamu ya wanafunzi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shule, Leon Malisa, alisema ombi hilo limetokana na kutambua mchango wa viongozi katika kuhamasisha maendeleo ya elimu na jamii kwa ujumla.

“Tunaamini akilikubali ombi hili, atakuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa wanafunzi wetu na maendeleo ya shule kwa ujumla,” alisema Malisa.

Aidha, bodi hiyo ilisisitiza umuhimu wa wazazi kushiriki kikamilifu katika vikao vya shule na kuchangia maendeleo, ikieleza kuwa ushirikiano kati ya wazazi na shule ni msingi wa mafanikio ya wanafunzi.

Pia, wahitimu wa kidato cha sita walihimizwa kusoma kwa bidii, kuzingatia nidhamu na kujiandaa vyema kwa mitihani yao ya mwisho ili kufikia malengo yao ya elimu ya juu.

Mahafali hayo yalihudhuriwa na wazazi, walezi, walimu na wadau mbalimbali wa elimu, huku yakiacha taswira ya matumaini makubwa kwa mustakabali wa Shule ya Sekondari Korona na wanafunzi wake.








Post a Comment

0 Comments