WAZIRI MKUU AAGIZA UJENZI UFANYIKE USIKU NA MCHANA, BARABARA ZA AFCON ARUSHA ZIKAMILIKE KWA WAKATI
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, amemuelekeza mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa barabara zinazoelekea katika Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Arusha (Uwanja wa AFCON) kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Ametoa agizo hilo leo Aprili 17, 2026, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo na miundombinu yake, akisisitiza kuwa muda uliobaki ni mfupi huku wakaguzi kutoka Confederation of African Football wakitarajiwa kuwasili kwa ajili ya ukaguzi kabla ya mashindano ya Africa Cup of Nations 2027.
Licha ya kueleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa katika baadhi ya maeneo ya mradi huo, Dk. Nchemba amesema kasi ya ujenzi wa barabara bado hairidhishi na inapaswa kuongezwa mara moja ili kuhakikisha zinakamilika kabla ya Mei 2026.
“Ni lazima mkandarasi aongeze nguvu kazi, vifaa na muda wa kazi. Nataka kuona kazi ikiendelea mchana na usiku bila kusimama ili tufikie viwango vinavyotakiwa kwa wakati,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Ameelekeza pia kuwa ujenzi wa barabara hizo uzingatie kikamilifu viwango vya ubora vinavyokidhi mahitaji ya kimataifa, akionya kuwa mapungufu yoyote yanaweza kuhatarisha hadhi ya nchi wakati wa ukaguzi wa CAF.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, miundombinu hiyo siyo tu kwa ajili ya mashindano, bali pia ni uwekezaji wa kudumu kwa wananchi wa Arusha, hivyo lazima izingatie thamani halisi ya fedha za umma na kurahisisha usafiri wa watu na huduma wakati na baada ya mashindano.
Katika hatua nyingine, ameitaka pia mamlaka husika kuhakikisha uwepo wa mifumo ya kisasa ya usalama ikiwemo kufungwa kwa kamera (CCTV) katika maeneo yote ya uwanja na viwanja vingine vitakavyotumika, ili kudhibiti vitendo visivyofaa na kuimarisha usalama wa mashabiki na wachezaji.
“Ninataka maeneo yote yawe na ulinzi wa kutosha wa kisasa. Hii itasaidia kuondoa vitendo visivyokubalika, ikiwemo imani potofu zinazoweza kuharibu taswira ya michezo yetu,” aliongeza.
Aidha, Waziri Mkuu alitoa onyo kali kwa wakandarasi wanaochelewesha miradi au kushindwa kulipa wafanyakazi wao kwa wakati, akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia uzembe wa aina hiyo.
“Mkandarasi yeyote atakayekiuka maelekezo ya Serikali, iwe kwa kuchelewesha kazi au kutowalipa wafanyakazi, hataruhusiwa kushiriki katika miradi mingine ya Serikali,” alionya.
Awali, Dk. Nchemba alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuharakisha maendeleo ya nchi, akibainisha kuwa ameweka msingi imara wa mageuzi ya kiuchumi na kijamii.
Alisema hatua ya Rais Samia kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya miaka 25 ijayo pamoja na maboresho ya mitaala ya elimu ni ya kihistoria, akifananisha na mageuzi makubwa yaliyowahi kufanywa enzi za Julius Kambarage Nyerere mwaka 1967.
Mradi wa uwanja wa AFCON na miundombinu yake unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya michezo, uchumi na utalii katika Jiji la Arusha na Taifa kwa ujumla.
Ends..





0 Comments