MADIWANI ARUSHA WAMKABIDHI RAIS SAMIA NG’OMBE WA MAZIWA KAMA ISHARA YA SHUKRANI
Na Joseph Ngilisho | Arusha
Madiwani wa Jiji la Arusha, wakishirikiana na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Paul Christian Makonda, wamemkabidhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, zawadi ya ng’ombe jike wa kisasa wa maziwa ikiwa ni ishara ya upendo, heshima na shukrani kwa mchango wake mkubwa katika kuleta maendeleo ndani ya jiji hilo.
Zawadi hiyo ya kipekee ilikabidhiwa rasmi katika hafla iliyofanyika mkoani Arusha, ambapo viongozi wa jiji hilo walieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kutambua juhudi za Rais Samia katika kuimarisha miundombinu, kukuza uchumi wa wananchi na kuendeleza mshikamano wa kijamii.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Makonda alimpongeza Rais Samia kwa uongozi wake thabiti na wenye matokeo chanya, akibainisha kuwa katika kipindi chake, Arusha imepata mafanikio makubwa kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi.
Alitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na uboreshaji wa barabara za ndani ya jiji, upanuzi wa huduma za kijamii pamoja na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya michezo, hususan maandalizi ya uwanja wa kisasa kwa ajili ya mashindano ya AFCON, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za ajira na kukuza uchumi wa eneo hilo.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba, pamoja na viongozi wengine wa serikali na chama, walioungana kwa pamoja kupongeza juhudi za Rais katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo nchini.
Kwa upande wao, madiwani wa Jiji la Arusha walisema zawadi hiyo ya ng’ombe wa maziwa inaashiria uzalishaji, ustawi na maendeleo endelevu, wakisisitiza kuwa wananchi wa Arusha wana imani kubwa na uongozi wa Rais Samia katika kuendelea kuwaletea maendeleo zaidi.
Hatua hiyo inaonesha wazi namna ambavyo viongozi na wananchi wa Arusha wanavyothamini mchango wa Rais Samia katika kuboresha maisha yao, huku ikidhihirisha mshikamano uliopo kati ya serikali na wananchi katika kujenga taifa lenye maendeleo jumuishi.
Ends..

0 Comments