WAWEKEZAJI WA MAREKANI WAZIDI KUMIMINIKA KASKAZINI, TISEZA YATOA MWELEKEO MPYA

 WAWEKEZAJI WA MAREKANI WAZIDI KUMIMINIKA KASKAZINI, TISEZA YATOA MWELEKEO MPYA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

Ukanda wa Kaskazini mwa Tanzania unaendelea kujitokeza kama kitovu kikuu cha uwekezaji nchini, huku zaidi ya kampuni 120 kutoka Marekani zikiwa zimewekeza mtaji wa zaidi ya dola milioni 180 na kuzalisha ajira zaidi ya 6,000 kwa Watanzania.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Kanuti Mosha, wakati wa mkutano wa wawekezaji uliofanyika jijini Arusha, ulioratibiwa na Chama cha Wafanyabiashara wa Marekani nchini (AmCham Tanzania).

Akizungumza katika mkutano huo, April 8,2026 Mosha alisema Kanda ya Kaskazini ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta za kilimo, utalii, viwanda na nishati, huku nafasi yake ya kijiografia ikiifanya kuwa lango muhimu la biashara na nchi jirani.

“Ukanda huu una mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi kutokana na rasilimali zake na miundombinu inayoendelea kuboreshwa. Hii ndiyo sababu wawekezaji wengi wanauona kama eneo lenye tija kubwa,” alisema Mosha.

Alieleza kuwa mwezi Machi mwaka huu, TISEZA ilisaini hati ya makubaliano (MOU) na AmCham Tanzania yenye lengo la kurahisisha huduma kwa wawekezaji wa Kimarekani na kuvutia uwekezaji zaidi nchini.


Kwa mujibu wa Mosha, uwekezaji wa Marekani umejikita zaidi katika sekta ya utalii, ambapo umechangia kuboresha huduma, kuimarisha miundombinu na kuitangaza Tanzania kimataifa. Aidha, umeenea katika sekta ya kilimo, hususan uzalishaji wa mazao ya bustani, ufugaji na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao.

Alisisitiza kuwa bado kuna fursa kubwa ambazo hazijatumika kikamilifu, akitoa mfano wa mazao ya matunda kama maembe yanayopotea wakati wa msimu kutokana na ukosefu wa viwanda vya usindikaji.

“Endapo tutapata wawekezaji wa kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao haya, tutaongeza thamani, kupunguza upotevu na kuimarisha ajira,” aliongeza.

Mosha alitaja maeneo ya Hanang na Arusha Vijijini kuwa na uhitaji mkubwa wa uwekezaji katika viwanda vya usindikaji wa mazao ya kilimo, sambamba na sekta za nishati mbadala na huduma za kifedha ambazo ni muhimu kwa ukuaji wa viwanda.

Alibainisha kuwa TISEZA imepokea maoni ya wawekezaji kuhusu changamoto zilizopo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali ili kuboresha zaidi mazingira ya biashara.

Aliwataka wawekezaji waliopo kupanua mitaji yao na kuwakaribisha wapya kuwekeza katika ukanda huo, akisisitiza kuwa Tanzania inaendelea kuwa kivutio kikubwa cha uwekezaji wa kimataifa.

“Mkutano huu ni mwanzo mzuri wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi. Tutaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia mitaji zaidi,” alihitimisha.

AMCHAM YASISITIZA USHIRIKIANO WA SEKTA BINAFSI NA SERIKALI

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya AmCham Tanzania, Geoffrey Daniel Mchangila, alisema ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali ni nguzo muhimu katika kukuza uwekezaji na maendeleo ya uchumi.

Alisema mkutano huo uliwaleta pamoja wawekezaji wa Marekani waliopo Kanda ya Kaskazini ili kujadili changamoto na fursa zilizopo, pamoja na kutafuta suluhisho la pamoja la kuchochea ukuaji wa uchumi.

“Tumekuja kuwakutanisha wawekezaji ili tujadili changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na mamlaka za serikali. Hii ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya uwekezaji,” alisema Mchangila.

Alifafanua kuwa AmCham Tanzania, iliyoanzishwa mwaka 2015, ina wanachama takriban 100 wakiwemo makampuni ya Marekani na yale ya Tanzania yenye mahusiano ya kibiashara na Marekani.

Kwa mujibu wa Mchangila, mkutano huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na ushiriki mpana wa wawekezaji na uwepo wa taasisi za serikali zilizotoa majibu ya moja kwa moja kwa baadhi ya changamoto zilizowasilishwa.

Aidha, alisema maboresho ya sera na mifumo ya uwekezaji yanayofanywa na serikali yameongeza uwazi na utabirika wa mazingira ya biashara, hatua inayochochea ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na Marekani.

“Tunajivunia kuona biashara kati ya Tanzania na Marekani ikiendelea kukua. Hii ni matokeo ya juhudi za serikali kusikiliza na kutatua changamoto za wawekezaji,” aliongeza.

Mchangila alisisitiza kuwa AmCham Tanzania itaendelea kuwa daraja kati ya wawekezaji na serikali kwa kuhakikisha changamoto zinawasilishwa na kufanyiwa kazi kwa wakati, huku ikihamasisha uwekezaji mpya na kukuza uliopo.

Aliongeza kuwa mchango wa sekta binafsi ni muhimu katika kufikia azma ya Tanzania kuwa na uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050, hivyo akasisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wote wa maendeleo.

Kwa mujibu wake, utekelezaji wa makubaliano kati ya AmCham Tanzania na TISEZA umeanza kuzaa matunda, ukiwemo kufanyika kwa mkutano huo wa Arusha uliowawezesha wawekezaji kukutana moja kwa moja na wadau wa serikali.

Alibainisha kuwa jitihada hizo zinaashiria dhamira ya dhati ya serikali na sekta binafsi katika kujenga mazingira rafiki ya uwekezaji, yanayochochea ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa.




Ends 

Post a Comment

0 Comments