BAYO AITAKA SERIKALI KUIMARISHA UBIA NA SHULE BINAFSI KUKABILIANA NA MLIPUKO WA WANAFUNZI
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MWENYEKITI wa shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule Binafsi Tanzania (TAMONGSCO), Modesty Bayo, ameomba kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi kama suluhisho la haraka na la kudumu la changamoto ya uhaba wa nafasi za wanafunzi katika shule za umma.
Bayo alitoa kauli hiyo baada ya kufanya mazungumzo na Meya wa Jiji la Arusha, Maxmillian Matle Iranqhe, akisema kuwa ongezeko kubwa la wanafunzi linalotarajiwa katika miaka ijayo linahitaji mikakati ya pamoja na ya kimkakati ili kuepusha msongamano katika shule za Serikali.
Alieleza kuwa ziara yao ilikuwa na malengo mawili makuu; kutoa salamu za heshima kwa Meya na kujadiliana namna bora ya kuendeleza sekta ya elimu kupitia ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau binafsi.
“Tumefanya mazungumzo yenye tija na Mheshimiwa Meya, ambaye ametupatia maelekezo na ushauri muhimu kuhusu namna bora ya kuimarisha ushirikiano huu kwa manufaa ya wanafunzi na taifa kwa ujumla,” alisema Bayo.
Bayo alibainisha kuwa kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), kuna fursa kubwa ya kupunguza msongamano wa wanafunzi mashuleni, hususan ifikapo mwaka 2029 ambapo kutakuwa na ongezeko la wahitimu wa elimu ya msingi kutokana na mfumo wa “double cohort”.
Alifafanua kuwa mfumo huo utasababisha wanafunzi wengi kumaliza elimu ya msingi kwa wakati mmoja, hali itakayoongeza presha ya uhitaji wa nafasi katika shule za sekondari.
“Ni wazi kuwa Serikali peke yake inaweza kushindwa kumudu idadi hiyo kubwa ya wanafunzi. Tunapendekeza wanafunzi watakaokosa nafasi katika shule za Serikali waweze kujiunga na shule binafsi, huku Serikali ikichangia gharama za masomo yao,” alisisitiza.
Aidha, alitambua juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuboresha sekta ya elimu, akisisitiza kuwa ushirikiano huo utaongeza upatikanaji wa elimu bora na jumuishi kwa wanafunzi wengi zaidi nchini.
Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Arusha, Maxmillian Matle Iranqhe, aliahidi ushirikiano wa dhati kwa wamiliki wa shule binafsi, akisisitiza kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta hiyo katika kukuza elimu nchini.
Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa elimu ili kuhakikisha kunakuwepo na mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia, sambamba na kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu kwa watoto wote.
Mkutano huo umeelezwa kuwa sehemu ya jitihada za kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu nchini.
Ends..


0 Comments