Mahakama Yawahukumu Vijana Wawili Kwa Kuzusha Taarifa za Uongo, Wasababisha Shambulio la Raia
By Arushadigital | SUMBAWANGA
Mahakama ya Mwanzo ya Kipeta, Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, imewahukumu vijana wawili kifungo cha miezi sita jela kila mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuzusha taarifa za uongo zilizochochea vurugu na kuhatarisha usalama wa raia.
Waliohukumiwa ni Haruni William Mengo (24), mkazi wa Kalambazite, na Isack Simon Kaniki (19), mkazi wa Mshani. Hukumu hiyo ilitolewa Aprili 8, 2026 na Hakimu Wiligisi Mbunda baada ya mahakama kujiridhisha kuwa washtakiwa hao walitoa taarifa zisizo za kweli kwa nia ya kupotosha umma.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa, tukio hilo lilitokea Aprili 6, 2026 katika kijiji cha Mshani, ambapo vijana hao walidai kuwa wameibiwa sehemu zao za siri na kumtuhumu mtu asiyehusika, Issa Athumani Kidungwe (56), mkazi wa Handeni mkoani Tanga. Taarifa hiyo ya uzushi ilisababisha wananchi kumshambulia kwa kipigo, wakiamini madai hayo kuwa ni ya kweli.
Jeshi la Polisi lilifanya msako mara baada ya tukio hilo na kufanikiwa kuwakamata jumla ya watu saba wanaohusishwa na tukio hilo. Mbali na waliohukumiwa, watuhumiwa wengine watano bado wanashikiliwa huku taratibu za kisheria za kuwafikisha mahakamani zikiendelea.
Watuhumiwa hao waliobaki ni pamoja na Geofrey Milumba Deminic (24), Jafari Nebart Shanjila (25), Huruma Geofrey Kasonso (18), Costantino Octavian Kiatu (28) na Severino Cosmas Ngonyani (22).
Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa limetoa wito kwa wananchi kujiepusha na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, likisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa bila kuhatarisha maisha ya watu wasio na hatia.
Aidha, polisi wameonya kuwa hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayehusika na kusambaza au kuzusha taarifa za uongo zinazoweza kuvuruga amani na usalama a jamii.

0 Comments