POLISI ARUSHA WAWATAKA MABROKA WA MADINI KUZINGATIA SHERIA NA USALAMA KATIKA BIASHARA ZAO
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limewataka mabroka wa madini mkoani humo kuzingatia kikamilifu sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia biashara ya madini, likisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kudumisha usalama, kuzuia migogoro na kupambana na vitendo vya uhalifu vinavyoweza kujitokeza katika sekta hiyo.
Wito huo umetolewa leo na Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Salvas Makweli, wakati wa kikao maalum na wafanyabiashara wa madini kilichofanyika katika soko la madini jijini Arusha, chenye lengo la kutoa elimu ya utii wa sheria pamoja na kuimarisha uelewa kuhusu masuala ya usalama kazini.
Akizungumza katika kikao hicho, ACP Makweli alisisitiza kuwa uzingatiaji wa taratibu za kisheria katika biashara ya madini utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro miongoni mwa wadau na kudhibiti vitendo vya kihalifu vinavyoweza kuathiri utulivu wa jamii na uchumi kwa ujumla.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya madini ili kuhakikisha mazingira ya biashara yanakuwa salama, yenye uwazi na yanayozingatia misingi ya sheria za nchi.
Katika hatua nyingine, ACP Makweli aliwataka mabroka hao kujiepusha na imani potofu pamoja na vitendo vinavyokiuka maadili ya jamii, akieleza kuwa baadhi ya imani hizo zimekuwa zikichochea matukio ya ukatili, ikiwemo mauaji na vurugu zisizo za lazima.
Alitolea mfano wa kuenea kwa taarifa za uzushi kuhusu kupotea kwa viungo vya siri vya wanaume, akisisitiza kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote na zimekuwa zikisababisha hofu na taharuki katika jamii. Aliwataka wananchi kupuuza taarifa zisizo na uthibitisho na badala yake kufuata vyanzo rasmi vya taarifa.
Aidha, alionya kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kueneza taarifa za uongo au kujihusisha na vitendo vinavyochochea taharuki na uvunjifu wa amani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mabroka wa Madini Tanzania (CHAMMATA), Bw. Jeremia Kituyo, alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kutoa elimu hiyo muhimu, akiahidi kuwa wanachama wake wataendelea kuzingatia sheria, kushirikiana na vyombo vya dola na kutoa taarifa kwa wakati pale wanapobaini viashiria vya uhalifu.
Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya mabroka wa madini na Jeshi la Polisi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha biashara ya madini inakuwa salama, halali na yenye tija kwa taifa.
Ends..








0 Comments