WATENGENEZA MAUDHUI ZAIDI YA 450 WAPATIWA MAFUNZO ARUSHA, WASISITIZWA NIDHAMU YA FEDHA NA UWEKEZAJI

 WATENGENEZA MAUDHUI ZAIDI YA 450 WAPATIWA MAFUNZO ARUSHA, WASISITIZWA NIDHAMU YA FEDHA NA UWEKEZAJI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

Zaidi ya watengeneza maudhui 450 jijini Arusha, wakiwemo wasanii wa muziki na waigizaji, wamepatiwa mafunzo maalum yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kitaaluma ili waweze kunufaika na fursa za sekta ya ubunifu inayokua kwa kasi nchini.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, yalijikita katika kuwapa washiriki mbinu za usimamizi sahihi wa fedha, uwekezaji na matumizi bora ya mikopo wanayopata kupitia mfuko huo.



Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Haki za Wasanii, Dk. Asha Mshana, alisema kuwa ongezeko la watengeneza maudhui nchini linafungua fursa kubwa za ajira, lakini linahitaji nidhamu ya kifedha na uelewa wa kibiashara ili kuleta matokeo endelevu.

Alisisitiza kuwa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa unatoa mikopo kwa lengo la kuwawezesha wabunifu kukuza vipaji vyao na kujikwamua kiuchumi, akibainisha kuwa hakuna upendeleo katika utoaji wa mikopo hiyo.

“Ni wajibu wa wanufaika kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kurejesha kwa wakati ili kuendeleza mzunguko wa kuwainua wabunifu wengine,” alisema Dk. Mshana.

Mbali na masuala ya fedha, washiriki walihimizwa kuzingatia ubora wa maudhui, matumizi ya lugha za kimataifa ili kupanua soko, pamoja na kulinda maadili na taarifa binafsi wanapowasilisha kazi zao katika majukwaa ya kidijitali.

Kwa upande wake, Mhandisi Benezeth Kabunduguru kutoka Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia aliwataka washiriki kutumia ushawishi wao katika jamii kuhamasisha matumizi ya nishati safi, akisisitiza kuwa watengeneza maudhui wana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko ya fikra kwa jamii.

Alieleza kuwa kupitia ubunifu wao—ikiwemo video fupi, vichekesho na simulizi za maisha halisi—wanaweza kuelimisha jamii kwa urahisi kuhusu umuhimu wa kutumia nishati salama na rafiki kwa mazingira.

Aidha, alibainisha kuwa jitihada za kitaifa zinazoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan zinalenga kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, na hivyo kuwataka wabunifu kuunga mkono kampeni hiyo kwa vitendo.

Mafunzo hayo yanatajwa kuwa hatua muhimu ya kuwawezesha watengeneza maudhui zaidi ya 450 waliopata fursa hiyo, wakiwemo wasanii wa nyimbo na waigizaji, kujijenga kitaaluma na kiuchumi, na hatimaye kuchangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa ubunifu nchini.












Ends

Post a Comment

0 Comments