MTUHUMIWA AKIRI KUWAUWA WATOTO WANNE KWA MPIGO AKISAKA UTAJIRI

 Mauaji ya Kutisha Kampala: Mtuhumiwa Akiri Kuwaua Watoto Wanne kwa Imani ya Kupata Utajiri

Na ArushaDigital-UGANDA


Hali ya simanzi na taharuki imetanda nchini Uganda kufuatia tukio la kikatili lililotokea katika shule ya awali ya Ggaba, jijini Kampala, ambapo watoto wanne wasio na hatia walipoteza maisha baada ya kushambuliwa kwa visu.

Mtuhumiwa wa tukio hilo, Christopher Okello (39), ambaye ana uraia wa Uganda na Marekani, amekiri mbele ya vyombo vya sheria kuwa ndiye aliyehusika na mauaji hayo, akidai kuwa alifanya kitendo hicho kama sehemu ya kafara kwa lengo la kujipatia utajiri.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, Okello amefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka rasmi yanayomkabili, yakiwemo mauaji ya kukusudia. Waendesha mashtaka wameeleza kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 2, 2025, baada ya mtuhumiwa kufanikiwa kuingia katika eneo la shule hiyo kwa kujifanya mzazi wa mtoto anayesoma hapo.

Inadaiwa kuwa mara baada ya kuingia, alitumia mwanya huo kuwashambulia watoto kwa kutumia kisu, na kusababisha vifo vya watoto wanne papo hapo, huku wengine wakinusurika kwa majeraha na mshtuko mkubwa wa kisaikolojia.

Tukio hilo limeibua hisia kali kwa jamii ya Uganda na kimataifa, likizua mjadala mpana kuhusu usalama wa watoto mashuleni pamoja na kuongezeka kwa vitendo vya imani potofu vinavyohusishwa na tamaa ya utajiri wa haraka.

Mamlaka za usalama nchini humo zimeimarisha ulinzi katika shule mbalimbali huku uchunguzi zaidi ukiendelea kubaini iwapo mtuhumiwa alikuwa akishirikiana na watu wengine au la.

Wakati huo huo, familia za waathiriwa zinaendelea kuomboleza wapendwa wao waliopoteza maisha katika tukio hilo la kusikitisha, huku wito ukitolewa kwa jamii kuungana katika kupinga vitendo vya ukatili na kulinda haki na usalama wa watoto.

Post a Comment

0 Comments