SHIRIKISHO LA WAMILIKI SHULE BINAFSI LATARAJIA MKUTANO MKUU DODOMA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
SHIRIKISHO la Wamiliki na Mameneja wa Shule pamoja na Vyuo visivyo vya Serikali Tanzania Bara (TAMONGSCO),linatarajia kufanya Mkutano Mkuu wa kihistoria Aprili 15, 2026 jijini Dodoma, ukiwa na lengo la kuweka dira mpya ya maendeleo ya sekta ya elimu binafsi nchini.
Akitoa tamko rasmi jijini Arusha, Mwenyekiti wa shirikisho hilo, Modesty Bayo, alisema mkutano huo utakutanisha wadau muhimu wa elimu kutoka kote nchini wakiwemo wamiliki wa shule, mameneja wa taasisi za elimu na viongozi wa vyuo, katika kipindi ambacho sekta hiyo inapitia mageuzi makubwa ya sera na mifumo ya uendeshaji.
Bayo alieleza kuwa mkutano huo ni wa kipekee kutokana na kufanyika kwake mara baada ya Serikali kufanya maboresho muhimu kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, hatua inayotarajiwa kufungua ukurasa mpya wa majadiliano na maamuzi ya kimkakati kwa mustakabali wa elimu nchini.
“Mkutano huu utakuwa jukwaa muhimu la wadau kujadili kwa kina nafasi ya sekta binafsi katika kuinua ubora wa elimu na kuchangia maendeleo ya taifa,” alisema Bayo.
Katika kuongeza uzito wa mkutano huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi, ambapo atatoa hotuba itakayogusa mwelekeo wa sekta ya elimu na nafasi ya wawekezaji binafsi katika kuendeleza sekta hiyo.
Ajenda kuu zitakazojadiliwa ni pamoja na tathmini ya maendeleo ya shirikisho, mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba, kupokea wanachama wapya, pamoja na kujadili changamoto na fursa zilizopo katika uwekezaji wa elimu binafsi.
Aidha, Bayo amesisitiza umuhimu wa wanachama kushiriki moja kwa moja katika mkutano huo badala ya kusubiri taarifa za baadae, akieleza kuwa maamuzi yatakayofanyika yataathiri mustakabali wa taasisi zao na sekta nzima kwa ujumla.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, kwa sasa shirikisho linafanya kazi katika kanda tisa nchini likiwa na mtandao wa viongozi kuanzia ngazi ya kanda hadi wilaya, huku akiwataka viongozi hao kuongeza kasi ya uhamasishaji wa wanachama wapya ili kuimarisha mshikamano na nguvu ya pamoja.
Aliongeza kuwa sekta binafsi imeendelea kuwa mshirika muhimu wa Serikali kupitia mfumo wa ubia wa sekta ya umma na binafsi (PPP), unaolenga kupanua fursa za elimu na kuboresha miundombinu ya kujifunzia.
Hata hivyo, alionya kuwa kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari ifikapo mwaka 2028, mahitaji ya miundombinu yataongezeka kwa kasi, hali inayotoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na changamoto hiyo.
“Tunashuhudia mahitaji makubwa ya shule, madarasa na huduma za elimu. Huu ni wakati sahihi kwa taasisi binafsi kushirikiana na Serikali kwa manufaa ya watoto wa Tanzania,” alisisitiza.
Akihitimisha, Bayo alisema shirikisho hilo limepata nguvu mpya na mwelekeo imara, huku akiwakaribisha wanachama wote kushiriki mkutano huo muhimu unaotarajiwa kufungua ukurasa mpya wa maendeleo ya elimu binafsi nchini.
Ends...


0 Comments