LHRC YAPINGA UTEUZI WA ANGELA KIZIGHA HADHARANI, YATAKA UFAFANUZI WA SERIKALI

 LHRC YAPINGA UTEUZI WA ANGELA KIZIGHA, YATAKA UFAFANUZI WA SERIKALI

By Arushadigital


KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (Legal and Human Rights Centre – LHRC) kimeibuka na msimamo mkali kupinga uteuzi wa Angela Kizigha kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kikieleza kuwa hatua hiyo inaibua utata wa kisheria unaohitaji ufafanuzi wa haraka.

Katika tamko lake, LHRC imeeleza kuwa uteuzi huo uliofanyika Aprili 2, 2026, unaonekana kwenda kinyume na masharti ya Mkataba wa Kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki wa 1999, hususan Ibara ya 50 inayosimamia vigezo vya uwakilishi katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Kwa mujibu wa kifungu hicho, wajumbe tisa wanaochaguliwa kuiwakilisha nchi katika EALA wanapaswa kutoka miongoni mwa watu ambao si wabunge wa mabunge ya kitaifa ya nchi husika. Hivyo, LHRC imeeleza kuwa uteuzi wa Kizigha unaibua mgongano wa wazi wa kisheria iwapo utazingatiwa kwa tafsiri ya moja kwa moja ya mkataba huo.

“Tanzania kama mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ina wajibu wa kuheshimu na kutekeleza kikamilifu masharti ya mkataba wake,” imeeleza sehemu ya tamko hilo, ikirejea pia malengo ya jumuiya yaliyowekwa chini ya Ibara ya 5 pamoja na kanuni za msingi zilizoainishwa katika Ibara ya 7.

Mbali na hilo, LHRC imeitaka Serikali kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu uhalali wa uteuzi huo, ili kuondoa sintofahamu iliyojitokeza kwa umma na wadau wa sheria.

Aidha, taasisi hiyo imeibua hoja nyingine kuhusu hadhi ya wabunge James Milya na Ng’waru Magembe ndani ya EALA, ikitaka maelezo ya wazi kuhusu nafasi zao katika mazingira ya sasa.

Hatua ya LHRC imekuja wakati mjadala wa kisheria na kisiasa ukiendelea kushika kasi, huku wadau mbalimbali wakisubiri kauli rasmi ya Serikali kuhusu uteuzi huo unaoibua tafsiri tofauti za kikatiba na kimkataba.

Ends

Post a Comment

0 Comments