ARUSHA YATOA MIKOPO YA SH. BILIONI 2.65 KUINUA WANANCHI KIUCHUMI

 ARUSHA YATOA MIKOPO YA SH. BILIONI 2.65 KUINUA WANANCHI KIUCHUMI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

Jiji la Arusha limeendelea kuonyesha dhamira ya dhati ya kukuza uchumi wa wananchi wake baada ya kutoa mikopo isiyo na riba ya asilimia 10 yenye thamani ya shilingi bilioni 2.65 katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Mikopo hiyo inalenga makundi maalum ya kijamii yakiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera za maendeleo zinazolenga kuwainua wananchi wa kipato cha chini.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Matle Iranghe, alisema kati ya fedha hizo, vikundi 120 vya wanawake vimepatiwa kiasi cha shilingi bilioni 1.632, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika shughuli za uzalishaji mali na biashara.

Kwa upande wa vijana, alisema vikundi 35 vimewezeshwa kwa mikopo ya shilingi milioni 530.5, huku vikundi 16 vya watu wenye ulemavu vikinufaika na shilingi milioni 102, hatua inayodhihirisha juhudi za jiji hilo kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma katika safari ya maendeleo.

Meya Iranghe alibainisha kuwa utoaji wa mikopo hiyo katika awamu hii umeboreshwa kwa kiwango kikubwa, hususan katika vigezo vya upatikanaji wake, jambo lililopanua wigo wa wanufaika. Alieleza kuwa tofauti na mfumo wa awali uliokuwa ukihusisha mafunzo ya muda mrefu ya wiki moja hadi sita, sasa jiji limeboresha mbinu kwa kutoa elimu elekezi kwa waombaji, hatua iliyoongeza ufanisi na kuharakisha upatikanaji wa mikopo hiyo.

“Tumebadilisha mfumo ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata fursa hii kwa wakati na wanaitumia kwa tija katika kukuza uchumi wao,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Meya huyo alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki ya kiuchumi na kusimamia sera zinazolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Alisema juhudi za serikali zimekuwa chachu ya kuimarika kwa mifumo ya utoaji wa mikopo katika ngazi za serikali za mitaa, hali iliyochochea upatikanaji wa fursa kwa makundi mbalimbali ya kijamii.

Aidha, alisisitiza kuwa Jiji la Arusha litaendelea kuboresha mifumo ya utoaji wa mikopo hiyo ili kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa kwa ufanisi zaidi, sambamba na kuongeza tija na matokeo chanya katika maisha ya wananchi.

Hatua hiyo inaifanya Arusha kuwa miongoni mwa majiji yanayoongoza katika utekelezaji wa mipango ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo nafuu, ikiwa ni mkakati wa kupunguza umaskini na kukuza uchumi shirikishi nchini.

Ends

Post a Comment

0 Comments