WAONGOZA WATALII WAPIGWA MSASA ARUSHA: WAZIRI KIJAJI ASISITIZA UTAALAMU, USALAMA WA WAGENI NA UTALII ENDELEVU
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amefungua rasmi mafunzo ya Waongoza Watalii kwa mwaka 2026, akisisitiza umuhimu wa utaalamu, usalama na uwajibikaji katika kuimarisha sekta ya utalii nchini.
Akizungumza jijini Arusha Aprili 18, 2026, Dkt. Kijaji alisema waongoza watalii ni nguzo muhimu katika sekta hiyo, kwa kuwa wao ndio wanaokutana na wageni mara tu wanapowasili nchini na kuwa nao kwa muda mrefu zaidi katika safari zao.
“Ni wazi kuwa ninyi ndio mabalozi namba moja wa utalii wetu. Jinsi mnavyowahudumia wageni ndivyo inavyojenga taswira ya Tanzania kimataifa,” alisema.
Alibainisha kuwa mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya utalii yanatokana na juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa chachu ya kukuza utalii kupitia kampeni mbalimbali zikiwemo filamu za Ziara ya Kifalme Tanzania (The Royal Tour) na Tanzania ya Kuvutia (Amazing Tanzania).
Kwa mujibu wa Waziri huyo, idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kwa asilimia 161 kati ya mwaka 2021 hadi 2025, huku mapato ya sekta hiyo yakiongezeka kwa asilimia 238.5 katika kipindi hicho.
“Mafanikio haya yanapaswa kulindwa na kuendelezwa. Ndiyo maana Serikali kwa kushirikiana na wadau kama Chama cha Wasafirishaji Watalii Tanzania (TATO) imeandaa mafunzo haya ili kuboresha huduma na kuongeza ushindani wa kimataifa,” alieleza.
Alisema mafunzo hayo yanaendana na malengo ya Serikali ya kufikia watalii milioni 8 na kuongeza mchango wa utalii katika Pato la Taifa hadi asilimia 20 ifikapo mwaka 2030.
Katika mafunzo hayo yenye kaulimbiu isemayo “Utaalamu, Usalama na Uongoza Watalii Wenye Uwajibikaji katika Maeneo ya Hifadhi Tanzania,” washiriki wanatarajiwa kuimarisha taaluma zao, kuongeza uelewa wa masuala ya usalama na kuboresha utoaji wa huduma kwa viwango bora vya kimataifa.
Dkt. Kijaji alisisitiza kuwa Tanzania ina ushindani mkubwa katika soko la kimataifa la utalii, hivyo ni lazima huduma zinazotolewa ziendane na hadhi ya nchi hiyo inayojulikana kama “Kituo Bora cha Safari za Utalii Duniani.”
Aidha, aliwakumbusha waongoza watalii umuhimu wa kuzingatia usalama wa wageni, hasa wanapokuwa katika hifadhi za taifa, akieleza kuwa wanabeba dhamana kubwa ya maisha ya watalii.
“Ni lazima muwe na uwezo wa kufanya maamuzi ya haraka na sahihi kila wakati. Kuzingatia taratibu za hifadhi si tu kunalinda wageni, bali pia kunahifadhi rasilimali zetu kwa vizazi vijavyo,” alisisitiza.
Waziri huyo alibainisha kuwa jumla ya waongoza watalii 2,000 wanashiriki mafunzo hayo kati ya 13,050 waliosajiliwa, akiwataka washiriki kuwa mabalozi wa maarifa kwa wenzao watakaokosa fursa hiyo.
Pia aliwakumbusha kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya kazi hiyo, ikiwa ni pamoja na kumiliki leseni halali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kijaji alisema Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa matukio makubwa ya kimataifa, yakiwemo Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Oktoba 2026, Fainali Kuu za Tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards Grand Final 2026) pamoja na mashindano ya AFCON 2027.
Alisema matukio hayo ni fursa adhimu kwa sekta ya utalii, hivyo aliwataka wadau kuanza maandalizi mapema kwa kubuni vifurushi maalum vya utalii vitakavyowavutia wageni watakaohudhuria matukio hayo.
“Ni muhimu kuvitangaza mapema ili wageni wajue kuwa wanapokuja kushiriki matukio haya, pia wanapata nafasi ya kipekee ya kutembelea vivutio vya Tanzania,” alisisitiza.
Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Kijaji aliwashukuru wadau wote waliofanikisha mafunzo hayo, hususan TATO pamoja na wadhamini mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza mafunzo hayo ili kuongeza ubora wa huduma na ushindani wa sekta ya utalii.
Ends .





0 Comments