WADAU WA UTALII WAPAZA SAUTI UJIO WA AFCON-2027, WATIA WASIWASI SUALA LA MIUNDO MBINU ARUSHA,WAHITAJI KUSHIRIKISHWA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
WADAU wa sekta ya utalii jijini Arusha wameibua wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya maandalizi ya miundombinu na huduma, wakihofia kuwa jiji hilo linaweza kupata aibu ya kimataifa kuelekea mashindano ya AFCON 2027 iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
Akizungumza kwa hisia kali katika mkutano wa mafunzo ya waongoza utalii Arusha ,yaliyofunguliwa na waziri wa maliasili na utalii ,Ashatu Kijaji , mmiliki wa kampuni ya utalii ya Sunny Safaris Limited, Feroz Suleiman, amesema licha ya matarajio ya kupokea wageni wengi, bado kuna changamoto lukuki zinazoweza kudhoofisha taswira ya jiji hilo na nchi kwa ujumla.
Amesema wazo la kuweza kuhudumia wageni zaidi ya mia tatu kwa siku linaonekana kuwa gumu kufikiwa kutokana na hali halisi ya miundombinu iliyopo sasa, akieleza kuwa bado kuna upungufu mkubwa wa taa za barabarani, msongamano wa magari,Toyo,Bajaj pamoja na uwepo wa magari chakavu yanayohatarisha usalama na mwonekano wa jiji.
“Hatuna maandalizi ya kutosha. Mfumo wetu wa usafiri bado ni dhaifu, kuanzia usafiri wa umma hadi bodaboda. Ukifika muda wa usiku hali inazidi kuwa mbaya. Hii inaweza kuleta taswira mbaya kwa wageni wetu,” alisema Firoz.
Aidha, amegusia pia changamoto ya uhaba wa huduma muhimu kama migahawa ya kisasa na ya kutosha kuhudumia wageni, akisisitiza kuwa sekta ya huduma ni sehemu muhimu ya mafanikio ya matukio makubwa ya kimataifa.
Firoz ameomba vyombo vya usalama hasa askari wa usalama barabarani kuanza maandalizi mapema kwa kushirikiana na wadau wengine ili kuimarisha udhibiti wa trafiki na kuhakikisha jiji linakuwa rafiki kwa wageni.
Katika hatua nyingine, ameipongeza Serikali chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha utayari wa kusikiliza kero za wadau, kufuatia ziara ya viongozi wa juu akiwemo waziri aliyefika Arusha kukutana na wadau wa utalii.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa bado kuna haja ya kuwepo kwa mawasiliano ya karibu zaidi kati ya Serikali na wadau ili kuweka mikakati madhubuti na ya haraka ya kuboresha miundombinu, huduma na mazingira ya biashara.
“Tusipojiandaa vizuri, tutapoteza mapato makubwa ya kodi na fursa za kiuchumi. Hili si jambo la kubeza—ni lazima tuchukue hatua sasa,” aliongeza.
Wadau hao wameitaka Serikali kuharakisha maboresho ya miundombinu ya usafiri, taa za barabarani, upangaji wa jiji pamoja na huduma za utalii ili kuhakikisha Arusha inakuwa tayari kupokea wageni wa kimataifa kwa hadhi inayostahili.




0 Comments