KAGANDA AINGIA RASMI KINYANG’ANYIRO CHA UBUNGE ISIMANI, CCM YAPATA WAGOMBEA 18
Na Joseph Ngilisho Arushadigital|IRINGA
Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda, amejiunga rasmi katika kinyang’anyiro cha kuwania ubunge wa Jimbo la Isimani, hatua inayoongeza ushindani Mkubwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuelekea uchaguzi mdogo utakaofanyika kujaza nafasi iliyoachwa wazi.
Nafasi hiyo imepatikana kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, William Vangimembe Lukuvi, kilichotokea Machi 25, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi za chama, jumla ya wanachama 18 wamejitokeza kuchukua na kurejesha fomu za kuomba ridhaa ya CCM kuwania nafasi hiyo. Zoezi hilo lilifanyika kwa siku mbili, kuanzia Aprili 17 hadi 18, 2026, likihitimishwa kwa mafanikio katika Wilaya ya Iringa Vijijini.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 18, 2026, Katibu wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini na Mkurugenzi wa Uchaguzi wilayani humo, Sure Mwasanguti, alisema miongoni mwa waliojitokeza, wanawake ni wawili huku wanaume wakiwa 16, hali inayoonyesha ushindani mkubwa ndani ya chama hicho.
Alieleza kuwa kukamilika kwa zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu kunafungua ukurasa mpya wa hatua zinazofuata, ikiwemo uchambuzi na uteuzi wa mgombea mmoja atakayebeba bendera ya CCM katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.
“Chama sasa kinaelekea katika hatua ya kuchuja majina ya waombaji ili kumpata mgombea mwenye sifa, uwezo na kukubalika na wanachama pamoja na wananchi wa Isimani,” alisema Mwasanguti.
Miongoni mwa waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ni Fred Fabian Ngajiro (Vunjabei), Festo Shemu Kiswaga, Asakwe Lameck Widambe, Arif Ally Abri, Eng. Sebastian Antony Kiyoyo, Tumaini Godwin Msowoya na Watende Gwerino Kiyagi.
Wengine ni Lazaro Francis Ngwira, David Evance Komba, Thobias Karlo Mwilapwa, Titho Maulilyo Cholobi, Emmanuela Kaganda Mtatifikolo, Claudio Francis Nzwaga, Josephat Gwelino Msambwa, Elias Lupituko Migodela Kazikuboma, Egidy Stanslaus Mkolwe, Dk. Abdallah Suleiman Lusasi pamoja na Tedson Johansery Ngwale.
Jimbo la Isimani sasa lipo katika hatua ya kusubiri maamuzi ya vikao vya juu vya CCM vitakavyochambua majina hayo na hatimaye kumpata mgombea atakayewania kiti hicho katika uchaguzi mdogo ujao.
Uchaguzi huo unatarajiwa kuwa na ushindani mzito, ukizingatiwa idadi ya wagombea waliojitokeza ndani ya chama hicho kikuu cha siasa nchini.
DC Kaganda atakumbukwa kwa uongozi wake wenye tija na weledi unaosimamia utu na haki akiwa mkuu wa wilaya katika wilaya ya Arumeru na Babati na maeneo mengine hapa nchini.
..Ends..

0 Comments