USHIRIKIANO WA SEKTA WAPEWA NGUVU, WAIBUKA NGUZO YA MAFANIKIO YA AFYA MOJA
By Arushadigital |MOROGORO
SERIKALI imesisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya sekta mbalimbali ndiyo msingi mkuu wa mafanikio ya utekelezaji wa dhana ya Afya Moja, mfumo unaolenga kulinda afya ya binadamu, wanyama na mazingira kwa pamoja.
Akizungumza Aprili 1, 2026 mkoani Morogoro wakati wa kikao kazi cha tathmini ya Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Afya Moja (2022–2027), Mkurugenzi Msaidizi wa Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. Salum Manyatta, alisema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wananufaika na mpango huo kuanzia ngazi ya mikoa hadi taifa kupitia utekelezaji shirikishi.
Kikao hicho kilichoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Kitengo cha Afya Moja kwa kushirikiana na Shirika la CIHEB Tanzania, kimewakutanisha wadau mbalimbali kwa lengo la kufanya tathmini ya kina ya utekelezaji wa mpango huo na kuandaa mwelekeo wa hatua zijazo.
“Tunafanya tathmini ya kina ili kubaini utekelezaji wa Afya Moja katika sekta zote, kuanzia taasisi za serikali hadi wadau wa maendeleo. Tunataka kujua nini kimefanyika, mafanikio yaliyopatikana na maeneo yanayohitaji kuboreshwa. Hii itakuwa msingi muhimu wa Mpango Mkakati ujao wa mwaka 2028,” alisema Dkt. Manyatta.
Kwa upande wake, Mratibu wa Afya Moja na Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Kizoonotiki kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Gwakisa John, alieleza kuwa sekta ya afya imeendelea kushirikiana kwa karibu na sekta nyingine katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na yale yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Alitaja baadhi ya magonjwa hayo kuwa ni pamoja na kichaa cha mbwa na kimeta, akibainisha kuwa udhibiti wake umeimarika kutokana na ushirikiano kati ya sekta za afya, mifugo na mazingira chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu.
Hata hivyo, alikiri kuwepo kwa changamoto katika utekelezaji wa mpango huo, hususan katika mifumo ya ubadilishanaji taarifa serikalini.
“Bado kuna hitaji la kuboresha mifumo ya mawasiliano ya taarifa baina ya taasisi. Lakini kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, juhudi zinaendelea kuhakikisha mifumo yote ya serikali inaunganishwa ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa taarifa,” alisisitiza Dkt. Gwakisa.
Aliongeza kuwa sekta ya afya inaendelea kutafuta rasilimali kupitia maandiko ya miradi na ushirikiano na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha utekelezaji wa Afya Moja unakuwa endelevu na wenye matokeo chanya kwa jamii.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Afya Moja na Mratibu wa Mradi wa Usalama wa Afya Duniani unaotekelezwa na CIHEB Tanzania, Dkt. Irene Masawe, alisema ndani ya siku nne za kikao hicho, washiriki wamefanikiwa kupitia kwa kina maeneo muhimu ya utekelezaji wa mpango huo.
Alitaja maeneo hayo kuwa ni uratibu, ufuatiliaji, utekelezaji na tafiti, akieleza kuwa tathmini hiyo imetoa taswira halisi ya mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Wataalam ya Afya Moja katika eneo la Utafiti na Maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Dkt. Maurice Mbunde, alisema matokeo ya tathmini yanaonesha mafanikio makubwa yaliyotokana na ushirikiano madhubuti kati ya serikali na wadau wa maendeleo.
Alibainisha kuwa uratibu thabiti unaofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu umechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Afya Moja kwa kiwango cha kuridhisha.
Kwa ujumla, kikao hicho ni sehemu ya jitihada za serikali za kuhakikisha mipango mikakati ya kitaifa inafanyiwa tathmini ya mara kwa mara ili kuongeza tija, ufanisi na ubora wa huduma za afya pamoja na kuimarisha usimamizi wa majanga nchini.








0 Comments