DC MKUDE APUNGUZA KERO KWA ASILIMIA 85 ARUSHA,WANANCHI WAMPONGEZA,MAMA AINGIA VITANI NA MWANAYE KUGOMBEA MALI SUALA LATINGA KWA DC
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
HATUA ya Serikali ya Wilaya ya Arusha ya kusogeza huduma karibu na wananchi imeanza kuzaa matunda, baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Joseph Mkude, kutangaza kupungua kwa kero za wananchi kwa asilimia 85 tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa kuzisikiliza na kuzitatua moja kwa moja.
Akizungumza na vyombo vya habari katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mkude alisema mfumo huo unaotekelezwa kila Jumatano ya mwisho wa mwezi katika ngazi ya wilaya, na katikati ya mwezi katika ngazi ya kata, umeleta mapinduzi makubwa katika utatuzi wa changamoto za wananchi.
Alisema kuwa katika kikao cha hivi karibuni, jumla ya wananchi 16 waliwasilisha kero zao, nyingi zikiwa ni migogoro ya ardhi, mirathi na ajira, hususan kwa wafanyakazi wa viwanda na mashirika mbalimbali.
“Baadhi ya kero zinahusu masuala yaliyopo mahakamani, hivyo hatuwezi kuzitatua moja kwa moja, bali tunatoa mwongozo wa kufuata taratibu za kisheria ili haki ipatikane,” alieleza Mkude.
Aliongeza kuwa Serikali imejipanga kuimarisha utendaji katika ngazi za kata ili kuhakikisha changamoto nyingi zinapatiwa ufumbuzi mapema, na hivyo kupunguza msongamano wa kesi katika ngazi ya wilaya.
Mkude alibainisha kuwa moja ya changamoto zilizokuwa zikichochea kuongezeka kwa malalamiko ni kutokuwepo kwa hitimisho rasmi la baadhi ya migogoro, hali iliyosababisha kero kujirudia mara kwa mara.
“Hata kama suluhisho linaweza kuwa gumu kwa upande mmoja, ni lazima liandikwe rasmi na pande zote zikubaliane ili kuhitimisha mgogoro husika,” alisisitiza.
Alieleza kuwa ushirikiano kati ya wataalamu wa sheria, maendeleo ya jamii pamoja na huduma za msaada wa kisheria (Legal Aid) umeongeza ufanisi na kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa wakati.
Wananchi wa Jiji la Arusha wameeleza kuridhishwa na utaratibu huo, wakisema umeondoa adha ya kuzunguka ofisi nyingi bila majibu.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, mkazi wa Arusha, Adolf Anthony Msele, alisema mfumo huo umeleta matumaini mapya kwa wananchi waliokuwa wamekata tamaa kufuatilia haki zao.
“Kwa kweli tumefurahishwa sana. Sasa tunasikilizwa na kupatiwa majibu bila gharama yoyote. Hii imetupa faraja kubwa,” alisema Msele.
Aliongeza kuwa mgogoro aliouwasilisha ulikuwa umedumu kwa muda mrefu bila suluhisho, lakini kupitia jukwaa hilo ameanza kuona dalili za kupata haki yake.
“Nilishapoteza matumaini, lakini sasa naona mwanga wa suluhisho la kudumu,” alisema.
Simulizi ya Mama wa watoto 10 yaibua hisia.
Katika hali iliyogusa wengi, Mama Rose Lota Siara, mkazi wa Arusha na mama wa watoto kumi, aliwasilisha kero yake akilalamikia kunyanyaswa na mmoja wa watoto wake kufuatia mgogoro wa mali.
Mama huyo alisema baada ya kufiwa na mumewe mwaka 2020, aliachwa na mali zikiwemo nyumba na maduka, lakini mtoto wake ameanza kuingilia umiliki wa mali hizo kwa njia zisizo halali.
“Nililea na kusomesha watoto wangu kwa taabu kubwa, sikutegemea kufikia hatua ya kunyanyaswa na mtoto wangu mwenyewe,” alisema kwa huzuni.
Alisema ameamua kufikisha suala hilo kwa Mkuu wa Wilaya ili apatiwe haki na kulindwa dhidi ya vitendo hivyo, akionesha imani kubwa kwa mfumo huo mpya wa utatuzi wa kero.
Imani ya wananchi yaongezeka
Kwa ujumla, wananchi wamepongeza juhudi za uongozi wa wilaya kwa kusogeza huduma karibu nao, wakisema hatua hiyo imeongeza imani kwa serikali na kupunguza kwa kiasi kikubwa mlundikano wa malalamiko.
Mkude aliwataka wananchi kuendelea kutumia fursa hiyo kuwasilisha changamoto zao, akisisitiza kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake kwa wakati na bila vikwazo.
Ends...



0 Comments