MUUGUZI AFARIKI BAADA YA KUDAIWA KUCHOMWA KISU SAME KWA MGOGORO WA MAPENZI
Na ArushaDigital – SAME
Muuguzi msaidizi wa Hospitali ya Mji Same, Asha Bakari (25), amefariki dunia kufuatia tukio la kushambuliwa kwa kuchomwa kisu shingoni, linalodaiwa kuchochewa na wivu wa kimapenzi.
Tukio hilo limetokea usiku wa Aprili 20 katika makazi ya watumishi wa hospitali hiyo wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, na kusababisha taharuki kubwa miongoni mwa wafanyakazi na wakazi wa eneo hilo.
Akithibitisha tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa kimapenzi, ambapo marehemu alidaiwa kuwa na uhusiano na watu wawili.
“Inadaiwa mtuhumiwa, ambaye ni dereva bodaboda na aliyewahi kumsaidia marehemu katika masomo yake, alimuita kwa simu kabla ya kumshambulia kwa kisu,” amesema Mgeni.
Ameongeza kuwa mara baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alitoroka na kwamba jeshi la polisi linaendelea na msako mkali kumtia nguvuni, huku uchunguzi wa kina ukiendelea kubaini chanzo halisi cha tukio hilo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kisima, Kei Mbwambo, amelaani vikali tukio hilo akisema linatia doa taswira ya jamii na kuitaka jamii kuacha kujihusisha na vitendo vya ukatili vinavyotokana na migogoro ya mapenzi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya amani, maadili na utatuzi wa migogoro ili kuepusha matukio kama hayo yanayopoteza maisha ya watu.
Vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na uchunguzi huku mwili wa marehemu ukiwa umehifadhiwa kwa taratibu za kitabibu.
Ends

0 Comments