MBUNGE ARUMERU MAGHARIBI AITAKA SERIKALI KUTOA MAJIBU UJENZI SOKO LA NGARAMTONI
Na Joseph Ngilisho|DODOMA
MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Johannes Lukumay, ameibua hoja nzito bungeni akiitaka Serikali kueleza bayana ni lini itaanza ujenzi wa soko la kisasa katika eneo la Ngaramtoni, ahadi ambayo aliwahi kuitoa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa ziara yake mkoani Arusha.
Akiuliza swali hilo bungeni, Lukumay alisema wananchi wa Arumeru Magharibi wamekuwa na matarajio makubwa ya kunufaika na mradi huo muhimu, ambao unalenga kuboresha mazingira ya biashara na kuinua uchumi wa eneo hilo.
"Mh.spika Tarehe 1mwezi wa kumi,2025 rais samia suluhu Hasan alifanya ziara katika jimbo langu la Arumeru Magharibi na katika ziara hiyo aliahidi kujengwa kwa soko la kisasa eneo la Ngaramtoni,nilitaka kujua ni lini serikali itajenga soko hilo"
Alieleza kuwa licha ya ahadi hiyo kupokelewa kwa matumaini makubwa, bado hakuna utekelezaji unaoonekana, hali inayosababisha wananchi kuendelea kukosa huduma bora za soko na fursa stahiki za kibiashara.
“Mheshimiwa Spika, wananchi wa Ngaramtoni na maeneo jirani wanaendelea kufanya biashara katika mazingira yasiyoridhisha. Naomba Serikali ieleze ni lini hasa itaanza ujenzi wa soko la kisasa kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais,” alihoji Lukumay.
Mbunge huyo alisisitiza kuwa ujenzi wa soko hilo utakuwa chachu ya maendeleo kwa wakazi wa Arumeru Magharibi, hasa kwa kuwa eneo la Ngaramtoni ni kitovu muhimu cha shughuli za biashara na kilimo.
Aidha, alieleza kuwa uwepo wa soko la kisasa utasaidia kuongeza mapato ya Halmashauri, kuboresha usafi na usalama wa wafanyabiashara pamoja na kuvutia uwekezaji katika sekta ndogo na za kati.
Hoja hiyo imekuja wakati Serikali ikiendelea kusisitiza dhamira yake ya kuboresha miundombinu ya masoko nchini ili kuwawezesha wananchi kufanya biashara katika mazingira bora na yenye tija.
Wananchi wa Arumeru Magharibi sasa wanasubiri kwa hamu majibu ya Serikali pamoja na hatua za utekelezaji wa ahadi hiyo muhimu kwa maendeleo yao.

0 Comments