HUDUMA ZA TIBA KEMIKALI ZAANZA RASMI MOUNT MERU, MILA POTOFU ZALAUMIWA KUCHELEWESHA MATIBABU YA SARATANI

 HUDUMA ZA TIBA KEMIKALI ZAANZA RASMI MOUNT MERU, MILA POTOFU ZALAUMIWA KUCHELEWESHA MATIBABU YA SARATANI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA 

HUDUMA za tiba kemikali (chemotherapy) zimeanza rasmi kutolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru jijini Arusha, hatua inayotarajiwa kuboresha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa matibabu ya saratani na kupunguza adha kwa wagonjwa waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kutafuta huduma hizo.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo ulioambatana na kufunguliwa kwa Kituo cha Huduma za Saratani, Dk. Sarah Maongezi alisema pamoja na mafanikio hayo, bado mila potofu zinaendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa wagonjwa kufika hospitalini kwa wakati.

Dk. Maongezi, ambaye ni Meneja wa Mradi wa Saratani Afrika Mashariki kutoka Hospitali ya Aga Khan, alieleza kuwa baadhi ya wagonjwa huchelewa kuanza matibabu kutokana na imani zisizo sahihi, ikiwemo kutegemea tiba za kienyeji badala ya kutafuta huduma za kitabibu mapema.


“Saratani haisubiri. Mgonjwa anapaswa kuanza matibabu mara moja baada ya kugundulika ili kuongeza uwezekano wa kupona,” alisisitiza.


Alibainisha kuwa taasisi ya Aga Khan imechangia vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 58, vikiwemo viti maalum kwa wagonjwa, mashine ya kuchanganyia dawa za saratani pamoja na vifaa vya kusimamia utoaji wa tiba kemikali.


Mbali na hilo, taasisi hiyo imeendesha mafunzo kwa watoa huduma za afya, yakilenga kuboresha uwezo wa uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi, pamoja na kuimarisha tafiti na tathmini nchini Tanzania na Kenya.


Dk. Maongezi aliongeza kuwa huduma za kliniki tembezi zitaendelea kutolewa katika mikoa sita, ikiwemo Zanzibar, ili kuwafikia wananchi walioko maeneo ya mbali na huduma za afya.


Kwa upande wake, Dk. Harison Chuwa, bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Hospitali ya Aga Khan, alisema wataendelea kuwajengea uwezo wauguzi na wataalamu wa afya katika Hospitali ya Mount Meru ili kuhakikisha huduma hizo zinatolewa kwa ufanisi mkubwa.


Alisema kuanza kwa huduma za tiba kemikali kutapunguza mzigo kwa wagonjwa waliokuwa wakilazimika kusafiri kwenda Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam au Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro.


Aidha, Dk. Chuwa alieleza kuwa saratani ya mlango wa kizazi inaongoza kwa maambukizi nchini, huku saratani ya matiti ikiongezeka kwa kasi, hasa kwa wanawake walio chini ya miaka 40. Aliwahimiza wanawake na wasichana kujitokeza kwa wingi kufanya uchunguzi wa mara kwa mara.


Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha, Denis Rombo, aliwataka watoa huduma za afya kutoa huduma bora na zenye weledi kwa wagonjwa wote, akibainisha kuwa kuanza kwa huduma hizo kutaongeza idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa.


Alisema serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya hospitali hiyo ili kukabiliana na changamoto ya msongamano, akieleza kuwa kwa sasa kituo hicho kina vyumba saba vya kutolea huduma.


Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mount Meru, Dk. Alex Ernest, alisema kuanzishwa kwa huduma za saratani ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Arusha na maeneo jirani.


Alibainisha kuwa huduma hizo zitapunguza gharama kwa wagonjwa waliokuwa wakisafiri umbali mrefu, huku pia zikiongeza ufanisi wa utoaji wa huduma ndani ya hospitali hiyo.


Dk. Ernest alitoa shukrani kwa serikali na wadau mbalimbali, hususan kampuni ya Spanish Tiles kupitia Mkurugenzi wake Bobby Chadha, kwa kufadhili ujenzi wa kituo hicho.


Kwa upande wake, Chadha aliipongeza serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji yanayowezesha sekta binafsi kushiriki katika maendeleo ya jamii, hususan katika sekta ya afya.


Uzinduzi wa huduma hizo unatajwa kuwa hatua muhimu katika kupunguza vifo vinavyotokana na saratani kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za matibabu karibu na wananchi.









Ends..

Post a Comment

0 Comments