DC KARANGA ATEMBELEA ATHARI ZA MVUA ENDALA–CHEMCHEM, ATOA AGIZO ZITO KUHARAKISHA UJENZI WA MADARAJA
Na Joseph Ngilisho| KARATU
MKUU wa Wilaya ya Karatu, Mhe. Dkt. Lameck Karanga, ametoa maelekezo mazito kwa taasisi za serikali kuharakisha hatua za dharura na za muda mrefu za kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na mvua kubwa katika Kijiji cha Endala–Chemchem, akisisitiza kuwa wananchi hawapaswi kuendelea kuteseka kutokana na kukatika kwa mawasiliano ya barabara.
Akiwa katika ziara ya ukaguzi iliyofanyika Aprili 10, 2026, DC Karanga alijionea hali halisi ya uharibifu wa barabara ya mzunguko (Bypass) inayounganisha Manyara Kibaoni, Endala hadi barabara ya Mbulu, ambapo maeneo kadhaa yamekatizwa na mito na kufanya usafiri kuwa wa hatari na usiotabirika.
“Hali niliyoiona si ya kuvumilika. Serikali haitakubali wananchi wa Endala na maeneo jirani waendelee kukosa huduma za msingi kwa sababu ya miundombinu dhaifu. Tumejipanga kuhakikisha hatua za haraka zinachukuliwa kurejesha mawasiliano haya muhimu,” alisisitiza DC Karanga.
Katika ziara hiyo, aliambatana na wataalamu kutoka TARURA na TANESCO, pamoja na viongozi wa vijiji, tarafa ya Endabash na wananchi, ambapo kwa pamoja walipitia maeneo korofi yaliyoathiriwa zaidi na mvua.
DC Karanga alieleza kuwa serikali imeanza mchakato wa kufanya upembuzi yakinifu wa kina utakaoweka msingi wa ujenzi wa madaraja imara katika maeneo yenye mito inayokatiza barabara hiyo, hatua inayolenga kuondoa kabisa changamoto ya kukatika kwa mawasiliano wakati wa mvua.
“Hatutaki suluhisho la muda mfupi. Tunahitaji miundombinu itakayodumu na kuhimili majanga ya asili kama haya. TARURA hakikisheni mnaanza haraka upembuzi yakinifu na kuleta majibu ya utekelezaji,” alielekeza.
Sambamba na hilo, alimwagiza Meneja wa TANESCO Wilaya ya Karatu kushughulikia kwa haraka changamoto za upatikanaji wa umeme katika vijiji vinavyopitiwa na mradi huo, akibainisha kuwa huduma hiyo ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Katika hatua nyingine, DC Karanga alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na serikali kwa kulinda miundombinu inayojengwa na kutoa taarifa mapema pindi wanapoona dalili za uharibifu unaoweza kuzuilika.
Akihitimisha ziara hiyo, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuiwezesha TARURA kuboresha miundombinu ya barabara nchini, akisema juhudi hizo zinafungua fursa mpya za maendeleo kwa wananchi wa maeneo ya vijijini ikiwemo Wilaya ya Karatu.









0 Comments