KUMBUKIZI YA SOKOINE YATIKISA MONDULI JUU,PAROKO BAIJUKYA AMTAJA KAMA SHUJAA ALIYEJITOA SADAKA KUPIGANIA TAIFA NA WANANCHI ATAKA TAIFA KUYAENZI MAONO YAKE .

  Na Joseph Ngilisho | MONDULI

PAROKO wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Fransisco Monduli Juu  wilayani humo,Arnold Baijukya amemtaja hayati Edward Moringe Sokoine kama kiongozi shujaa aliyejitoa sadaka kupigania maslahi ya wananchi na taifa lake bila woga, kwa kupambana na uhujumu uchumi na rushwa, huku akilitaka taifa kuyaenzi maono yake kwa vitendo badala ya kuyaishia kwenye maneno.

 

Kauli hiyo aliitoa wakati akiongoza ibada maalumu ya kumbukizi ya miaka 42 ya kifo cha kiongozi huyo iliyofanyika nyumbani kwake Monduli Juu, wilayani Monduli mkoani Arusha, ambapo mamia ya waombolezaji walijitokeza kushiriki, wakiwemo viongozi wa serikali, wanasiasa, viongozi wa dini pamoja na ndugu na jamaa.

Akihubiri katika ibada hiyo iliyojaa hisia na tafakari nzito, Padri Baijukya aliwashukuru wazazi wa hayati Sokoine kwa kuzaa na kulea kiongozi aliyekuwa na mchango mkubwa kwa taifa, akisema urithi wake bado unaishi mioyoni mwa Watanzania wengi.


“Tunawashukuru wazazi wa Sokoine waliolitunuku taifa kiongozi wa kipekee, aliyejitolea mchana na usiku kulitumikia taifa lake. Hadi leo anaendelea kukumbukwa kwa matendo yake mema. Tunahitaji viongozi wa aina hii katika kizazi cha sasa,” alisema Padri huyo kwa msisitizo.

Aliendelea kueleza kuwa maisha ya Sokoine yanabeba funzo pana la uongozi unaozingatia uadilifu, uwajibikaji na uzalendo wa kweli, akibainisha kuwa hizi ndizo nguzo muhimu za kujenga taifa lenye haki na usawa.

“Hayati Sokoine hakuwa kiongozi wa maneno matupu, bali alidhihirisha kwa vitendo dhamira yake ya dhati ya kuwatumikia wananchi. Alisimama kidete kupambana na rushwa, ubadhirifu na aina zote za unyonyaji, akihakikisha rasilimali za taifa zinalindwa kwa manufaa ya wote,” alifafanua.

Katika mahubiri yake, Padri Baijukya aliunganisha maisha ya kiongozi huyo na mafundisho ya Kikristo yanayohimiza upendo, mshikamano na kugawana kwa haki, akirejea mfano wa waumini wa kwanza waliokuwa wakiishi kwa umoja na kusaidiana bila ubinafsi.

Aidha, Padri Baijukya aliwataka viongozi wa sasa kuyaishi kwa vitendo maono na misingi aliyosimamia hayati Sokoine, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ndiko kutakakowajengea heshima na kumbukumbu njema kwa jamii hata baada ya kuondoka duniani.

“Viongozi wa leo wanapaswa kuyaishi yale aliyoyaamini Sokoine—uadilifu, uwajibikaji na kujitoa kwa wananchi—ili nao wakumbukwe kwa mema kama ilivyo kwa hayati Sokoine. Heshima ya kiongozi haijengwi kwa maneno, bali kwa matendo,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa kumbukizi ya Sokoine haipaswi kubaki kuwa tukio la kila mwaka la kukutana na kuzungumza, bali iwe chachu ya mabadiliko ya kweli katika jamii, hususan kwa viongozi na watumishi wa umma.

“Tunapomkumbuka leo, ni lazima tujihoji kwa dhati—je, tunaendeleza yale aliyoyasimamia? Je, tunapinga rushwa kwa vitendo au kwa maneno? Je, tunasimamia haki kwa kila Mtanzania bila upendeleo? Haya ndiyo maswali ya msingi tunayopaswa kuyajibu,” alisisitiza.

Ibada hiyo ilipambwa pia na salamu na kumbukizi kutoka kwa baadhi ya viongozi waliohudhuria, wakimuelezea Sokoine kama kiongozi shupavu, mzalendo na asiyeogopa kusema ukweli, hata pale ilipokuwa hatarini kwake binafsi.




Kwa upande wao, baadhi ya ndugu wa familia walitoa shukrani kwa wote walioshiriki ibada hiyo, wakisema kuwa kuendelea kukumbukwa kwa Sokoine ni ishara ya mchango wake mkubwa kwa taifa na kwamba wataendeleza kuhifadhi tunu na misingi aliyoiamini.

Kwa ujumla, kumbukizi ya hayati Sokoine imeendelea kuwa kielelezo hai cha uongozi bora nchini, huku ikiendelea kutoa funzo muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo juu ya umuhimu wa uadilifu, uwajibikaji na kujitoa kwa ajili ya ustawi wa taifa.

Hayati Sokoine alifariki kwa ajali ya gari Aprili 12, 1984, huko Dumila, mkoani Morogoro ambapo pia anakumbukwa kama shujaa wa uadilifu, mpambanaji wa rushwa, na kiongozi aliyesisitiza kilimo cha kufa na kupona.










Ends..

Post a Comment

0 Comments