SAMIA ATAJWA KUENZI KWA VITENDO MAONO YA SOKOINE
Na Joseph Ngilisho | MONDULI
MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ni miongoni mwa viongozi wa juu nchini wanaoenzi kwa vitendo urithi na maono ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani, hayati Edward Moringe Sokoine.
Dkt. Lukumay alitoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya miaka 42 ya kifo cha hayati Sokoine yaliyofanyika nyumbani kwake, Monduli Juu, wilayani Monduli mkoani Arusha, ambapo viongozi mbalimbali wa serikali na wananchi walikusanyika kumkumbuka kiongozi huyo mashuhuri.
Alisema hayati Sokoine alijijengea heshima kubwa kutokana na uadilifu, uzalendo na msimamo wake thabiti katika kusimamia rasilimali za taifa, hususan kupitia mapambano dhidi ya hujuma za uchumi na juhudi za kuhakikisha wananchi wanajitegemea kwa kilimo na uzalishaji wa chakula.
“Hayati Sokoine alikuwa kiongozi wa vitendo. Aliamini katika kufanya kazi kwa bidii, kupinga rushwa na kuhakikisha kila Mtanzania anashiriki katika kujenga uchumi wa nchi yake. Leo tunapoangalia uongozi wa Rais Samia, tunaona dhahiri jitihada za kuendeleza yale aliyoyaamini,” alisema.
Mbunge huyo alieleza kuwa katika sekta ya elimu, hayati Sokoine alitoa mchango mkubwa kwa kumshauri Rais wa awamu ya kwanza, Julius Kambarage Nyerere, kuimarisha upatikanaji wa elimu bure, hatua iliyowezesha Watanzania wengi, hususan kutoka jamii za pembezoni, kupata fursa ya kusoma.
Alisema kwa sasa, serikali ya Rais Samia imeendeleza dhamira hiyo kwa kuhakikisha elimu bila malipo inapatikana kuanzia ngazi ya awali hadi sekondari ya juu, huku ikiimarisha mikopo ya elimu ya juu na kuanzisha programu maalum za ufadhili wa masomo kwa wataalamu, hususan katika sekta ya afya.
Aidha, Dkt. Lukumay alikumbusha kuwa hayati Sokoine alisisitiza sana uzalishaji wa chakula na kujitegemea kiuchumi, akihamasisha wananchi kulima kwa bidii ili kuepuka utegemezi wa chakula kutoka nje ya nchi.
“Leo hii tunaona msisitizo huo ukiendelezwa kupitia sera na mikakati ya serikali ya awamu ya sita inayolenga kukuza kilimo na kuhakikisha usalama wa chakula nchini,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, alibainisha kuwa hayati Sokoine alikuwa mtetezi mkubwa wa haki na maendeleo ya wanawake, akiamini kuwa elimu kwa mtoto wa kike ni msingi wa maendeleo ya jamii nzima.
Maadhimisho hayo yalienda sambamba na ibada maalumu ya kumwombea marehemu Sokoine, ambapo viongozi mbalimbali wa serikali, ndugu na jamaa pamoja na wananchi walishiriki kwa pamoja katika dua na sala za kumuombea kiongozi huyo.
Katika ibada hiyo, viongozi wakiwemo wajane wa marehemu waliinama kwa heshima na kuweka mashada ya maua katika kaburi la hayati Sokoine, kabla ya kuendelea na maombi maalumu ya kumuombea, tukio lililogubikwa na hisia za huzuni na heshima kubwa.
Aliwataka Watanzania kuendelea kuuenzi urithi wa kiongozi huyo kwa vitendo, ikiwemo kufanya kazi kwa bidii, kudumisha uadilifu na kuipenda nchi yao.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi wa serikali, familia ya marehemu Sokoine pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Arusha, wakikumbuka mchango wake mkubwa katika ujenzi wa taifa.







0 Comments