USIFANYE KAZI KWA MAZOEA – RAS AWAONYA WATUMISHI ARUSHA
Na Joseph Ngilisho | Arusha
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Nguvila, amewataka watumishi wa Serikali katika Jiji la Arusha kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kuongeza bidii, uwajibikaji na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.Akizungumza leo Machi 13, 2026 katika kikao kazi na watumishi wa Serikali wa Jiji la Arusha, Dkt. Nguvila alisema Serikali inatarajia kuona watumishi wake wanakuwa chachu ya maendeleo kwa kuhakikisha huduma zinatolewa kwa wakati, kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
“Serikali haihitaji watumishi wanaofanya kazi kwa mazoea. Tunahitaji watu wanaofanya kazi kwa bidii, wanaowajibika na wanaotambua kuwa jukumu lao ni kuwatumikia wananchi kwa uadilifu,” alisema.
Katika kikao hicho kilicholenga kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi pamoja na kujadili njia za kuzitatua, Dkt. Nguvila alisisitiza umuhimu wa viongozi na watumishi kuchukua hatua mapema katika kushughulikia changamoto ndogo ndogo kabla hazijageuka kuwa matatizo makubwa.
Akitumia msemo maarufu wa Kiswahili, “Usipoziba ufa utajenga ukuta,” alifafanua kuwa watumishi wanapaswa kuwa makini katika kutatua matatizo yanayoibuka katika maeneo yao ya kazi ili kuzuia madhara makubwa ambayo yanaweza kuathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.
Dkt. Nguvila alibainisha kuwa Jiji la Arusha linahitaji watumishi wenye maono na mipango madhubuti ya kazi, wanaoweza kushughulikia kwa haraka changamoto za wananchi na kuhakikisha maendeleo ya jiji hilo yanaendelea kwa kasi inayotarajiwa.
Aidha, alionya kuwa hatakuwa tayari kuvumilia uzembe, kutowajibika au tabia ya baadhi ya watumishi kutoa visingizio badala ya kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Katika hatua nyingine, Katibu Tawala huyo alisisitiza umuhimu wa kujenga mahusiano mazuri kati ya viongozi wa ngazi mbalimbali pamoja na watumishi, akieleza kuwa ushirikiano na mawasiliano mazuri ni msingi muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
“Umoja, mshikamano na mawasiliano mazuri kazini ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya Serikali ya kuwahudumia wananchi kwa ufanisi,” alieleza.
Aidha aliwataka watumishi wa umma kuendelea kushirikiana kwa karibu na wananchi katika maeneo yao ya kazi ili kuhakikisha kero zinazowakabili zinasikilizwa na kupatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Alisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wa Jiji la Arusha wanapata huduma bora na stahiki, hivyo ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kuchochea maendeleo ya Jiji la Arusha na Mkoa wa Arusha kwa ujumla.
Kikao hicho ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma za umma kwa wananchi katika ngazi za mikoa na halmashauri.
Ends..







0 Comments