DR LUKUMAY: SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA HUDUMA ZA TIBA YA SARATANI, WANANCHI KUNUFAIKA NA MATIBABU BILA MALIPO

 MWENYEKITI KAMATI YA BUNGE: SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA HUDUMA ZA TIBA YA SARATANI, WANANCHI KUNUFAIKA NA MATIBABU BILA MALIPO

Na Joseph Ngilisho – Arushadigital | DAR ES SALAAM



MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, amesisitiza dhamira ya Serikali kuimarisha huduma za matibabu ya magonjwa sugu ikiwemo saratani, akieleza kuwa wagonjwa watanufaika na huduma hizo bila malipo kulingana na maelekezo ya Rais.

Dkt. Lukumay alitoa msisitizo huo leo Machi 13, 2026 jijini Dar es Salaam baada ya kuongoza wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo ya sekta ya afya, ikiwemo kutembelea Hospitali ya Amana pamoja na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

Katika ziara hiyo, kamati hiyo ilipata fursa ya kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati inayolenga kuimarisha huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani nchini, miradi inayotekelezwa chini ya Wizara ya Afya kupitia Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

Miradi iliyokaguliwa na kamati hiyo ni pamoja na mradi wa mashine za tiba ya mionzi za LINAC na Cobalt 2, mradi wa vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa saratani vya PET/CT Scan pamoja na Cyclotron, pamoja na ujenzi wa Jengo la Multi-Purpose Oncology ambalo linatarajiwa kuongeza uwezo wa utoaji huduma za matibabu ya saratani kwa wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Lukumay alisema uwekezaji unaofanywa na Serikali katika sekta ya afya ni sehemu ya juhudi za dhati za kuboresha huduma za matibabu ya magonjwa sugu nchini, hasa saratani ambayo imekuwa ikiathiri idadi kubwa ya wananchi.

Alieleza kuwa kamati hiyo imefurahishwa na maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo na kusisitiza kuwa kukamilika kwake kutasaidia kupunguza changamoto za upatikanaji wa huduma za uchunguzi na tiba ya saratani ambazo hapo awali zilikuwa zikiwalazimu baadhi ya wagonjwa kusafiri nje ya nchi au kukumbana na gharama kubwa za matibabu.

Katika ziara hiyo pia, Mwenyekiti huyo alipata fursa ya kuzungumza moja kwa moja na baadhi ya wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, ambapo walieleza changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo, ikiwemo gharama kubwa za matibabu ya saratani.

Akijibu hoja hizo, Dkt. Lukumay aliwahakikishia wagonjwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka kipaumbele katika kuboresha huduma za afya, hususan kwa wagonjwa wa magonjwa sugu.

Alisema tayari Rais ametoa maelekezo kuwa matibabu ya magonjwa sugu ikiwemo saratani yaendelee kuimarishwa na kutolewa bila malipo kwa wagonjwa wanaostahili, sambamba na utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unaolenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya bila kikwazo cha kifedha.

Dkt. Lukumay alisisitiza kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi na sera za sekta ya afya ili kuhakikisha dhamira ya Serikali ya kuwapatia wananchi huduma bora za afya inafikiwa.







Ends..

Post a Comment

0 Comments