Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Maandalizi ya kuelekea Mkutano Mkuu wa Chama cha Maafisa Michezo Tanzania (TASOA) unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha yameanza kupata nguvu zaidi baada ya wadau mbalimbali wa michezo, wakiwemo taasisi za kifedha, kuanza kujitokeza kuunga mkono mkutano huo kwa kutoa misaada mbalimbali.
Miongoni mwa wadau waliojitokeza kuunga mkono maandalizi ya mkutano huo ni Benki ya Diamond Trust Bank (DTB) pamoja na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ Bank), ambazo zimeanza kuchangia vifaa vitakavyosaidia kufanikisha maandalizi ya mkutano huo wa kitaifa.
Katika hatua ya awali, Makamu wa Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Michezo Tanzania (TASOA), Benson Maneno, amepokea msaada wa T-shirt 50 kutoka Benki ya DTB ikiwa ni sehemu ya mchango wa wadau wa michezo katika kuhakikisha mkutano huo unafanyika kwa mafanikio.
Msaada huo umekabidhiwa rasmi Machi 12, 2026 katika ofisi za benki hiyo jijini Arusha, tukio lililoonyesha dhamira ya sekta binafsi kushiriki katika kukuza na kuendeleza michezo nchini kupitia taasisi zake za kitaaluma.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Afisa Mauzo wa Benki ya DTB, Jazary Shaha, alisema benki hiyo imeamua kuunga mkono mkutano huo kwa kutambua nafasi muhimu ya maafisa michezo katika kuendeleza sekta ya michezo nchini.
Alieleza kuwa DTB ni mdau muhimu katika maendeleo ya jamii, hususan katika sekta ya michezo, na kwamba benki hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha shughuli za michezo nchini.
“Tunatambua mchango mkubwa wa maafisa michezo katika kusimamia na kuendeleza michezo nchini, hivyo tumeona ni vyema kuunga mkono juhudi hizi kuelekea mkutano mkuu wa TASOA. Aidha, tunaamini maandalizi haya pia yana mchango katika kujenga mazingira mazuri kuelekea mashindano makubwa ya AFCON 2027 yatakayofanyika katika nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania,” alisema Shaha.
Aidha, alitoa wito kwa wadau wa michezo pamoja na wananchi kwa ujumla kufungua akaunti katika benki hiyo ili kuendelea kuimarisha huduma za kifedha na kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo michezo.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa TASOA Benson Maneno alishukuru wadau hao kwa mchango wao, akisema ushiriki wa taasisi za kifedha na wadau wengine ni muhimu katika kufanikisha maandalizi ya mkutano huo na shughuli nyingine za maendeleo ya michezo nchini.
Mkutano Mkuu wa TASOA unatarajiwa kufanyika kuanzia Machi 28 hadi 30, 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa AICC jijini Arusha, ukihusisha maafisa michezo kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Katika mkutano huo, washiriki wanatarajiwa kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya michezo, usimamizi wa shughuli za michezo katika ngazi za serikali za mitaa, pamoja na nafasi ya maafisa michezo katika kuimarisha miundombinu na programu za michezo nchini.
Ends..



0 Comments