MWENYEKITI WA KAMATI YA BUNGE AIPONGEZA SERIKALI KUINUA WANAKONGA KIUCHUMI
Ataka masoko ya bidhaa zao yaboreshwe ili kuongeza tija
Na Joseph Ngilisho | DAR ES SALAAM
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, ambaye pia ni Mbunge wa Arumeru Magharibi, Mhe. Johannes Lukumay, ameipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuendelea kuwawezesha watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (Wanakonga) kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kujikwamua kimaisha.
Mhe. Lukumay alitoa pongezi hizo Machi 19, 2026 baada ya Kamati hiyo kufanya ziara ya kutembelea na kujionea shughuli za Baraza la Watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI katika Kongamano la Konga ya Jiji, lililofanyika katika Viwanja vya Pugu Mnadani jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI wanapaswa kupewa nafasi sawa na wananchi wengine katika fursa za maendeleo, akisisitiza kuwa wana uwezo mkubwa wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi iwapo watawezeshwa ipasavyo.
“Wanakonga ni sehemu muhimu ya jamii na wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi na kuzalisha. Ni wajibu wetu kuhakikisha wanapata fursa sawa na msaada unaohitajika ili waweze kufanikiwa,” alisema Mhe. Lukumay.
Aidha, aliwapongeza wanakonga kwa juhudi zao za kujikwamua kiuchumi kupitia miradi mbalimbali ya uzalishaji mali, huku akiitaka Serikali na wadau kuhakikisha wanawatafutia masoko ya uhakika kwa bidhaa zao ili kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.
Kwa upande wake, Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Mhe. Ummy Nderiananga, alisema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuimarisha juhudi za kuwawezesha wanakonga kiuchumi.
Alisisitiza kuwa Serikali itaongeza nguvu katika kuwajengea uwezo na kuwaunganisha na fursa mbalimbali za kiuchumi ili kuhakikisha wanakuwa sehemu ya maendeleo jumuishi ya taifa.
“Mhe. Rais ameweka msisitizo mkubwa katika kuwainua wananchi wote kiuchumi, wakiwemo wanakonga. Tutahakikisha wanapata msaada unaohitajika ili waweze kusimama imara kiuchumi,” alisema.
Katika hatua nyingine, alimpongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya pamoja na Katibu Tawala wa Halmashauri ya Jiji kwa juhudi zao za kuwawezesha wanakonga kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Aliwataka kuendelea na moyo huo, akibainisha kuwa bado kuna nafasi ya kuongeza nguvu katika utekelezaji wa mipango hiyo kabla ya mwaka wa fedha kumalizika.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, alisema kuwa jiji hilo limeweka mkazo katika kuimarisha shughuli za Konga kwa kuwaunga mkono kiuchumi na kitaalamu ili kuhakikisha wanapata mafanikio endelevu.
Aliongeza kuwa uwezeshaji wa makundi maalum ni hatua muhimu katika kujenga jamii jumuishi na kupunguza umasikini, huku ukichochea maendeleo ya kweli kwa wananchi wote.
Ends..







0 Comments