MAAFISA 9 WA POLISI WALIOKUWA WAKIMLIMDA BOBI WINE WASHTAKIWA ,HATARINI KUFUKUZWA KAZI KWA UZEMBE WA ULINZI WA BOBI WINE

 MAAFISA 9 POLISI HATARINI KUFUKUZWA KAZI KWA UZEMBE WA ULINZI WA BOBI WINE

Na Arushadigital 

Maafisa tisa wa Jeshi la Polisi waliokuwa wamepewa jukumu maalum la kumlinda kiongozi wa Chama cha National Unity Platform (NUP), Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, wanakabiliwa na hatua kali za kinidhamu baada ya kushtakiwa kwa makosa ya kutotii amri pamoja na uzembe kazini.

Taarifa zilizothibitishwa zinaeleza kuwa maafisa hao walifikishwa mbele ya Kitengo cha Nidhamu cha Polisi Machi 12, 2026, ambacho kipo chini ya Kurugenzi ya Kupambana na Ugaidi, kufuatia madai ya kushindwa kutekeleza ipasavyo majukumu yao ya ulinzi kulingana na maelekezo ya kazi waliyopewa.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani, uchunguzi wa awali umebaini kuwapo kwa mapungufu makubwa katika utekelezaji wa majukumu yao, hali iliyotajwa kuhatarisha usalama wa kiongozi huyo wa kisiasa pamoja na taswira ya taasisi ya polisi kwa ujumla.

Vyanzo vya kuaminika ndani ya jeshi hilo vinaeleza kuwa maafisa hao wanatuhumiwa kupuuza taratibu za kiusalama, kushindwa kufuata miongozo ya ulinzi, pamoja na kuonesha uzembe uliokiuka maadili ya kazi za kipolisi. Kutokana na uzito wa tuhuma hizo, mapendekezo yametolewa ya kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu, ikiwemo kufukuzwa kazi kwa baadhi yao endapo watapatikana na hatia.

Aidha, hatua hiyo inaelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za Jeshi la Polisi kuhakikisha nidhamu, uwajibikaji na weledi vinazingatiwa miongoni mwa askari wake, hasa katika majukumu nyeti yanayohusu ulinzi wa viongozi wa kisiasa na watu mashuhuri.

Wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema tukio hilo linapaswa kuwa funzo kwa vyombo vya dola kuimarisha mafunzo, ufuatiliaji na tathmini ya utendaji kazi kwa askari wanaopewa majukumu ya ulinzi, ili kuepusha matukio yanayoweza kuhatarisha usalama wa watu na mali.

Hadi sasa, Jeshi la Polisi halijatoa taarifa rasmi kuhusu hatma ya mwisho ya maafisa hao, huku uchunguzi wa kina ukiendelea kubaini ukweli wa tuhuma zinazowakabili.

Post a Comment

0 Comments