ACE DIAMOND YATOA MSAADA WA T-SHIRT 50 KWA TASOA KUENDELEA MAANDALIZI YA MKUTANO MKUU ARUSHA,MANENO AIMWANGIA SIFA

ACE DIAMOND YATOA MSAADA WA T-SHIRT 50 KWA TASOA KUENDELEA MAANDALIZI YA MKUTANO MKUU ARUSHA

 Na Joseph Ngilisho | ARUSHA



Makamu wa Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Michezo Tanzania (TASOA), Benson Maneno, amepokea msaada wa awali wa T-shirt 50 kutoka Kampuni ya Ace Diamond, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Maafisa Michezo Tanzania unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha mwishoni mwa mwezi huu.


Msaada huo umekabidhiwa leo Machi 11, 2026 jijini Arusha, ukiwa ni mchango wa wadau wa michezo katika kuhakikisha maandalizi ya mkutano huo yanafanyika kwa ufanisi na mafanikio.


Mkutano huo wa kitaifa wa TASOA unatarajiwa kufanyika kuanzia Machi 28 hadi 30, 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa AICC jijini Arusha, ukihusisha maafisa michezo kutoka mikoa mbalimbali nchini watakaokutana kujadili masuala muhimu yanayohusu maendeleo na usimamizi wa michezo nchini.


Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo, Makamu Mwenyekiti wa TASOA, Benson Maneno, aliishukuru Kampuni ya Ace Diamond kwa ushirikiano na mchango wao katika kusaidia kufanikisha maandalizi ya mkutano huo muhimu kwa sekta ya michezo.


Alisema mchango huo unaonesha namna wadau wa sekta binafsi wanavyoendelea kushirikiana na taasisi za michezo katika kuimarisha maendeleo ya michezo nchini.


“Tunawashukuru Ace Diamond kwa moyo wao wa kujitolea kusaidia maandalizi ya mkutano huu. Ushirikiano wa wadau kama wao ni muhimu sana katika kuhakikisha sekta ya michezo inaendelea kukua na kuimarika,” alisema Maneno.


Aidha, alibainisha kuwa mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu kwa maafisa michezo kutoka maeneo mbalimbali nchini kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto zinazowakabili pamoja na kuweka mikakati mipya ya kuendeleza michezo katika ngazi zote.


Kwa upande wao, wadau wa michezo wanaendelea kuhamasishwa kushirikiana na TASOA katika maandalizi ya mkutano huo, ambao unatarajiwa kukutanisha wataalamu wa michezo na viongozi mbalimbali wa sekta hiyo kutoka pande tofauti za nchi.


Mkutano Mkuu wa TASOA unatajwa kuwa moja ya mikutano muhimu inayolenga kuimarisha taaluma ya uamuzi na usimamizi wa michezo nchini Tanzania, sambamba na kukuza ushirikiano kati ya maafisa michezo na wadau wengine wa maendeleo ya michezo.


Ends...

Post a Comment

0 Comments