WAZIRI MAKONDA: UJENZI WA UWANJA WA AFCON ARUSHA WAFIKIA ASILIMIA 75

WAZIRI MAKONDA: UJENZI WA UWANJA WA AFCON ARUSHA WAFIKIA ASILIMIA 75

 Na Joseph Ngilisho | ARUSHA


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu unaotarajiwa kutumika katika mashindano ya Africa Cup of Nations (AFCON) unaoendelea jijini Arusha umefikia asilimia 75 ya utekelezaji.


Waziri Makonda alitoa kauli hiyo leo Marchi 12,2026 wakati akizungumza na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo iliyofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo mkubwa wa kimataifa.


Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Makonda alisema kazi nyingi muhimu za ujenzi zimefanyika kwa kiwango kikubwa, ikiwemo uwekaji wa zege (concrete), ufungaji wa vyuma na kazi za upigaji plasta ambazo kwa kiasi kikubwa tayari zimekamilika.


“Kwa ujumla mradi umefikia asilimia 75, lakini ukiangalia kwa undani baadhi ya kazi zimefikia hatua kubwa zaidi. Zipo zilizokamilika kwa zaidi ya asilimia 90, nyingine asilimia 78 na nyingine asilimia 75, jambo linaloonesha kuwa ujenzi unaendelea vizuri,” alisema Makonda.


Aidha, Waziri huyo aliishukuru Serikali kwa kuhakikisha fedha za mradi zinapatikana kwa wakati, hali ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kasi ya ujenzi huo na kumwezesha mkandarasi kuendelea na kazi bila vikwazo.


“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa wakati. Hii imesaidia mkandarasi kuendelea na kazi zake kwa ufanisi na kuhakikisha mradi unaenda kwa kasi iliyopangwa,” alisisitiza.


Katika hatua nyingine, Makonda alieleza kuwa maboresho mbalimbali ya miundombinu yanafanyika ili kuhakikisha uwanja huo unakuwa na mazingira bora kwa wachezaji na mashabiki.

Alifafanua kuwa awali kulikuwa na mpango wa timu zote kuingia kupitia lango moja, jambo ambalo lingeweza kusababisha changamoto za kiusalama na msongamano.


 Hata hivyo, baada ya ushauri wa wataalamu na kamati husika, mpangilio huo umeboreshwa na sasa kila timu itakuwa na njia na lango lake maalum la kuingia na kutoka.


Kwa upande wa huduma muhimu, Waziri huyo alisema Serikali imeanza kutekeleza miradi ya maji, umeme na mawasiliano katika eneo la uwanja ili kuhakikisha miundombinu yote muhimu inapatikana kwa wakati.


Alibainisha kuwa tayari maandalizi ya ujenzi wa tenki kubwa la maji yameanza ili kuhakikisha uwanja huo unakuwa na uhakika wa upatikanaji wa maji wakati wote.


Kuhusu miundombinu ya barabara, Makonda alisema Serikali kupitia mamlaka husika imepanga kujenga na kuboresha barabara mbalimbali zitakazorahisisha upatikanaji wa uwanja huo kwa mashabiki na wageni watakaohudhuria michezo ya AFCON.


Alisema barabara kadhaa zitaunganisha uwanja huo na maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha, huku nyingine zikipanuliwa ili kupunguza msongamano wa magari wakati wa mashindano.


“Lengo la Serikali si kujenga uwanja pekee, bali kuhakikisha miundombinu yote muhimu inaimarishwa ili mashabiki, wachezaji na wageni watakaokuja kushuhudia mashindano ya AFCON waweze kufika kwa urahisi na usalama,” alisema Makonda.


Mashindano ya AFCON yanatarajiwa kuipa Tanzania fursa kubwa ya kukuza sekta ya michezo, utalii na uchumi kwa ujumla, huku uwanja huo wa Arusha ukiwa miongoni mwa miradi muhimu inayotekelezwa kwa maandalizi ya mashindano hayo makubwa barani Afrika.









Ends...

Post a Comment

0 Comments