MBUNGE ARUMERU MAGHARIBI AKERWA NA UTEKELEZAJI DHAIFU WA MAAGIZO YA RC MAKALLA NI KUHUSU MABORESHO YA BARABARA YA SAMBASHA,OLMOTONY NA NGARAMTONI

 MBUNGE ARUMERU MAGHARIBI AKERWA NA UTEKELEZAJI DHAIFU WA MAAGIZO YA RC MAKALLA

Asema baadhi ya halmashauri zinafanya kazi ya “Copy and Paste”, azitaka TARURA na TANROADS kushughulikia haraka miundombinu iliyoharibiwa na mvua

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Kukumay, ameonyesha kukerwa na kile alichokiita uzembe wa baadhi ya halmashauri katika Mkoa wa Arusha kwa kushindwa kutekeleza kikamilifu maagizo ya Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla, kuhusu kushughulikia changamoto za miundombinu ya barabara zinazowaathiri wananchi hasa katika kipindi hiki cha mvua za masika.

Akizungumza katika Kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC) kilichohusisha pia Bodi ya Barabara ya Mkoa, Dkt. Kukumay aliwataka viongozi wa halmashauri kushirikiana kwa karibu na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ili kuhakikisha changamoto za barabara zinatatuliwa kwa haraka na kwa ufanisi.

Mbunge huyo alionyesha kutoridhishwa na namna baadhi ya watendaji wanavyotekeleza majukumu yao, akidai kuwa badala ya kufanya kazi ya vitendo wanajikita katika kuwasilisha taarifa zisizoendana na hali halisi ya maeneo.

“Baadhi ya halmashauri wanaonekana kufanya kazi ya ‘copy and paste’, wakati wananchi wanahitaji suluhisho la kweli la changamoto za miundombinu. Ni muhimu maagizo ya Mkuu wa Mkoa yakatekelezwa kwa vitendo ili kuleta tija kwa wananchi,” alisisitiza Dkt. Kukumay.

Katika maelezo yake, Dkt. Kukumay alitaja baadhi ya maeneo yenye changamoto kubwa ya barabara katika jimbo lake, akielekeza kuwa hatua za haraka zichukuliwe kuboresha miundombinu hiyo.

Alizitaja kata za Sambasha, Olmotony na Ngaramtoni kuwa miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na hali mbaya ya barabara, hasa kipindi hiki cha mvua ambapo maji hukusanyika barabarani na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu.


Kwa mujibu wa mbunge huyo, baadhi ya barabara zimekuwa na mashimo makubwa na makorongo yanayohatarisha usalama wa wananchi na hata kufanya baadhi ya maeneo kushindwa kupitika kwa urahisi.

Dkt. Kukumay alisisitiza umuhimu wa kuchimbwa kwa mitaro ya maji kando ya barabara ili kupunguza mkusanyiko wa maji ya mvua barabarani, jambo ambalo kwa muda mrefu limekuwa chanzo kikuu cha uharibifu wa barabara katika maeneo hayo.

Alionya kuwa endapo hatua za haraka hazitachukuliwa, hali ya miundombinu itaendelea kuwa mbaya zaidi na kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii za wananchi.

“Wananchi wanahitaji barabara zinazopitika muda wote ili kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa. Hivyo mamlaka husika zinapaswa kuchukua hatua za haraka kabla hali haijawa mbaya zaidi,” aliongeza.

Kauli ya mbunge huyo imekuja wakati ambapo Mkoa wa Arusha unakabiliwa na mvua za masika zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali, hali inayosababisha baadhi ya barabara kuharibika na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wa miundombinu hiyo.

Wadau wa maendeleo katika kikao hicho walisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya halmashauri, TARURA na TANROADS ili kuhakikisha barabara zinaboreshwa kwa wakati na kupunguza adha wanazokumbana nazo wananchi kila msimu wa mvua.

Ends..

Post a Comment

0 Comments