WAZIRI MKUU AAGIZA UCHUNGUZI WA FEDHA ZA MRADI WA OFISI YA MKUU WA WILAYA KITETO
Na Joseph Ngilisho — KITETO
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemtaka Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Bahati Haule, kufanya uchunguzi wa kina na kuwasilisha taarifa ya mtu mmoja mmoja aliyedaiwa kuhusika katika kuchukua fedha za mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kiteto.
Akizungumza Alhamisi leo, Februari 26, 2026, mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi hiyo, Waziri Mkuu alisema kurejeshwa kwa fedha pekee hakutoshi, bali hatua za kinidhamu lazima zichukuliwe kwa watumishi wote waliobainika kuhusika ili kulinda misingi ya uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za umma.
Alisema ofisi hiyo inatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 1.85 hadi kukamilika kwake, huku ujenzi ukiwa umefikia asilimia 85.
“Kamanda wa TAKUKURU, ninataka uniletee taarifa hii kabla sijamaliza ziara yangu katika Mkoa wa Manyara. Nahitaji taarifa za mtu mmoja mmoja kwa wote waliohusika kuchukua fedha hizo. Hatukutumwa kuja kuchukua fedha za umma; hatua za kinidhamu lazima zichukuliwe,” alisisitiza.
Aidha, Waziri Mkuu alielekeza kuwasilishwa kwa taarifa ya kina kuhusu mapato ya ndani ya halmashauri, yakiwemo mapato yatokanayo na minada, ili kubaini namna yanavyokusanywa na kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Alisisitiza kuwa Serikali haitavumilia ubadhirifu wa mali ya umma, akitaka uwazi na nidhamu ya fedha kuzingatiwa katika ngazi zote za utendaji.
“Hakuna kuvumilia ubadhirifu wa mali ya umma. Tunataka kila mtu aheshimu fedha za utekelezaji wa miradi,” aliongeza.







0 Comments