TANZANIA YAOMBWA KUREJEA KWENYE ITIFAKI YA MAHAKAMA YA AFRIKA NA HAKI ZA BINADAMU,ILI KUWAPA UHURU WANANCHI WAKE KUDAI HAKI ZA KISHERIA KATIKA MAHAKAMA HIYO

 TANZANIA YAOMBWA KUREJEA UTARATIBU WA RAIA KUFUNGUA MASHAURI MOJA KWA MOJA MAHAKAMA YA AFRIKA

Na Joseph Ngilisho –ARUSHA. 


MAHAKAMA ya Afrika ya Haki za Binadamu (AfCHPR)na Watu imeiomba Tanzania kurejea katika tamko linaloruhusu wananchi binafsi kufungua mashauri moja kwa moja katika mahakama hiyo ya kikanda, hatua inayotajwa kuwa muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa haki na uwajibikaji wa kisheria nchini.

Wito huo umetolewa Februari 26,2026 jijini Arusha, wakati wa mkutano wa wadau wa haki za binadamu uliofanyika jijini hapa, sambamba na maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa mahakama hiyo yenye jukumu la kutafsiri na kusimamia utekelezaji wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu wa mwaka 1981.


Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dkt. Anna Henga, alisema kurejea kwa Tanzania katika utaratibu huo kutafungua milango kwa wananchi kudai haki zao za msingi kwa ufanisi zaidi na kuimarisha mifumo ya kitaifa ya sheria.

Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, mahakama hiyo imekuwa jukwaa muhimu la kushughulikia masuala nyeti ikiwemo haki za uchaguzi, haki za wanawake, uhuru wa kujieleza na mijadala ya adhabu ya kifo barani Afrika.

 Aidha, alibainisha kuwa utekelezaji wa hukumu zake umechangia mageuzi ya kisheria na kisera katika mataifa kadhaa wanachama.


Washiriki wa mkutano huo walisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya serikali za Afrika na taasisi za haki za binadamu ni nguzo muhimu katika kuimarisha utawala wa sheria, demokrasia na heshima kwa haki za msingi. 

Walieleza kuwa mazingira thabiti ya kisiasa na kiuchumi yana mchango mkubwa katika utekelezaji wa maamuzi ya mahakama za kikanda.

Mkutano huo uliwakutanisha wataalamu wa sheria, wanaharakati na vijana kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika pamoja na mashirika ya kimataifa, ikiwemo Office of the High Commissioner for Human Rights, kwa lengo la kujadili utekelezaji wa hukumu na mchango wake katika kuboresha mifumo ya haki barani.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama Cha Wanasheria wa Afrika, Donald Deya, alisema mkutano wa siku mbili na nusu wa wadau wa haki za binadamu unalenga kutathmini mafanikio, changamoto na mwelekeo wa mahakama hiyo katika kulinda haki za watu na jamii barani Afrika.

Alisema katika kipindi cha miongo miwili, mahakama hiyo imekuwa chombo muhimu cha kutoa maamuzi yanayolinda haki za binadamu, huku wadau wakitathmini pia kiwango cha utekelezaji wa hukumu zake katika nchi wanachama.

Kwa mujibu wa Deya, baada ya mkutano huo wadau wanatarajiwa kushiriki ufunguzi rasmi wa kikao cha kwanza cha mahakama kwa mwaka huu, ambapo hukumu mbalimbali zitatolewa, zikiwemo kesi zinazohusu Tanzania.

Deya alitoa wito kwa serikali ya Tanzania kurejesha tamko linaloruhusu wananchi kufungua mashauri moja kwa moja katika mahakama hiyo, akisema hatua hiyo itaongeza hadhi ya nchi kimataifa na kuimarisha utawala wa sheria.

Kwa sasa, Watanzania wanaowasilisha malalamiko kuhusu ukiukwaji wa haki hulazimika kupitia African Commission on Human and Peoples’ Rights yenye makao yake makuu Banjul, nchini Gambia, badala ya kufungua mashauri moja kwa moja katika mahakama hiyo.

Hata hivyo, Deya alibainisha kuwepo kwa dalili chanya kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonyesha utayari wa kulitazama upya suala hilo, huku juhudi za kidiplomasia zikiendelea kushawishi kurejeshwa kwa utaratibu huo.

Wadau walisisitiza kuwa ushiriki kamili wa Tanzania katika mahakama hiyo utaimarisha nafasi ya nchi katika kuongoza juhudi za kulinda haki za binadamu barani Afrika na kutoa mfano kwa mataifa mengine katika kuimarisha utawala wa sheria.

Kwa pamoja, walitoa wito kwa serikali ya Tanzania na nchi nyingine wanachama kuendelea kushirikiana kikamilifu na mahakama hiyo ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kwa mujibu wa viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.







...Ends..

Post a Comment

0 Comments