BALTON TANZANIA YAZINDUA VIUATILIFU 10 KUPAMBA NA WADUDU NA MAGONJWA, KUONGEZA UZALISHAJI WA MAZAO
Na Joseph Ngilisho, ARUSHA
KAMPUNI ya Balton Tanzania imezindua viuatilifu 10 vipya vinavyolenga kuwasaidia wakulima wa ngano, mahindi, kahawa, korosho, nyanya, vitunguu, maharage na mbogamboga kudhibiti wadudu, magonjwa na magugu, hatua inayotarajiwa kuongeza uzalishaji wa mazao na kuchangia uhakika wa chakula nchini.
Uzinduzi huo ulifanyika mbele ya wauzaji wakubwa wa pembejeo za kilimo, ambapo viongozi wa kampuni hiyo walisema bidhaa hizo zimeundwa kwa teknolojia ya kisasa ili kupunguza usugu wa wadudu na kusaidia mazao kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuathiri uzalishaji katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Jacob Vorster, alisema viuatilifu vipya vina ubora wa juu na vinalenga kumaliza changamoto ya wakulima kukosa mavuno ya kutosha kutokana na wadudu, magonjwa na pembejeo zisizo na ufanisi sokoni.
“Kwa mara ya kwanza tumeleta viuatilifu vyenye uwezo mkubwa wa kudhibiti wadudu na magugu, huku vikisaidia mazao kustahimili mabadiliko ya tabianchi. Lengo ni kuongeza tija kwa mkulima na kuhakikisha uzalishaji endelevu wa chakula,” alisema Vorster.
Alibainisha kuwa bidhaa hizo zitasambazwa nchi nzima kupitia mtandao wa mawakala wa kampuni hiyo ili kuwafikia wakulima wengi kwa wakati.
Kwa upande wake, mtaalamu wa sayansi ya mimea wa kampuni hiyo, Chonya Wema, alifafanua kuwa miongoni mwa viuatilifu vilivyozinduliwa ni pamoja na OMEGA 112EC kinachodhibiti wadudu waharibifu kama inzi weupe, thrips na funza katika mazao mbalimbali ikiwemo nyanya, mahindi na vitunguu.
Alitaja bidhaa nyingine kuwa ni AZOXY Plus 325EC inayodhibiti magonjwa ya kuvu kama ukungu unga na kutu ya majani; Balton Tebu 250EC inayosaidia ukuaji na afya ya mazao ya ngano, kahawa na viazi; pamoja na ANERIX Extra 76WP inayolenga viazi, mikorosho na mbogamboga.
Viuatilifu vingine ni HALO Plus 60EC kwa mazao ya nyanya na mpunga, NICO Plus 300OD kwa mahindi, RIBEME 75WDG kwa ngano na shayiri, LUZAFEN 250EC kwa maharage, MWANZO 660SE ya kudhibiti magugu kabla ya kuota mazao na TENO Super 75 inayolenga ngano na shayiri.
Kwa mujibu wa Wema, bidhaa hizo zimepangwa kuuzwa kwa bei nafuu na katika maeneo yote ya nchi, zikiwa na lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha uchumi wa wakulima.
Baadhi ya mawakala wa pembejeo za kilimo walipongeza hatua hiyo lakini wakashauri kuwepo kwa ujazo tofauti wa bidhaa hizo ili kuwapa wakulima wadogo fursa kubwa zaidi ya kuzimudu.
Akizungumza kwa niaba ya mawakala, Swalehe Mkilindi kutoka Moshi alisema viuatilifu hivyo vina matumaini ya kuwa suluhisho kwa wakulima wanaokabiliwa na ongezeko la wadudu na magugu mashambani.
Alisema upatikanaji wa pembejeo bora utasaidia kuongeza mavuno, kipato cha wakulima na kuchochea ukuaji sekta ya kilimo nchini.
MWISHO











0 Comments