Serikali Yasisitiza Kuongeza Kasi ya Miradi ya Maji Safi Nchini
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
SERIKALI imeagiza mamlaka zote za maji nchini kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji safi na usafi wa mazingira, huku ikisisitiza uwajibikaji wa karibu, matumizi ya teknolojia za kisasa, na ulinzi wa vyanzo vya maji ili huduma ifikie wananchi kwa uhakika na kwa viwango vinavyokubalika.
Akifungua Mkutano wa Bodi za Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji Safi na Usafi wa Mazingira jana katika Hotel ya Ngurdoto, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba alisema bodi za mamlaka za maji zina wajibu wa kutoa mwelekeo wa kimkakati, kusimamia thamani ya fedha za umma, na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.
“Maji ni uhai na msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Bodi na watendaji wanapaswa kuacha mazoea yasiyo na tija na kuzingatia matokeo yanayopimika.” alisisitiza Dkt. Nchemba.
Alionya dhidi ya uharibifu wa vyanzo vya maji na vitendo vya kujiunganishia maji kinyume cha sheria, huku akimtaka Waziri wa Maji kudhibiti upotevu wa maji na kuimarisha usimamizi wa miundombinu.
“Tukichezea vyanzo vya maji, hata kama fedha zipo, tutakosa maji. Si jambo zuri kusikia wananchi wanakosa maji huku maji yakienda hovyo. Kagueni miundombinu yetu ya usambazaji ili tukomeshe upotevu,” aliongeza.
Aidha, Waziri Mkuu alibainisha kuwa Serikali imeshanunua mitambo ya kuchimba na kusambaza maji katika kila ukanda wa nchi ili kila mkoa uwe na mtambo wake. Alisisitiza kuwa mamlaka za maji zinapaswa kutumia mitambo hiyo na magari yaliyotolewa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji haraka.
“Tunataka kila shule ya msingi na sekondari, zahanati, na vituo vya afya viwe na maji. Hii inaweza kufanikishwa kupitia miradi ya kisima au mitambo ya maji. Tunapoongeza uwekaji wa maji katika shule na vituo vya afya, tunachangia maendeleo ya jamii na afya ya wananchi,” alisema Dkt. Nchemba.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Juma Aweso, alisema mageuzi ya sekta ya maji yameongeza upatikanaji wa huduma, huku maeneo ya mijini yakifikia zaidi ya asilimia 90. Alieleza kuwa matumizi ya mita za malipo kabla (pre-paid meters) yameongeza uwazi, kupunguza malalamiko ya bili, na kuboresha ukusanyaji wa mapato.Aweso pia aliongeza kuwa Serikali imepanua wigo wa fedha kupitia ushirikiano na sekta binafsi na matumizi ya hati fungani za kijani (Green Bonds), sambamba na miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo usambazaji wa maji kutoka Ziwa Victoria na maandalizi ya kutumia maji ya Ziwa Tanganyika katika maeneo yenye changamoto sugu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri, alisema Tanzania ina mamlaka 85 za maji, na bodi zake ni kiungo muhimu kati ya sera na utekelezaji. Alisisitiza umuhimu wa mafunzo ya uongozi, usimamizi wa miradi, na uwajibikaji wa taasisi ili kuongeza ubora na uendelevu wa huduma.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andelile, alibainisha kuwa uimara wa huduma za maji unategemea moja kwa moja ufanisi wa bodi za wakurugenzi. Alisisitiza kuweka vigezo madhubuti vya utendaji kwa menejimenti na kulinda maslahi ya wananchi kupitia huduma bora na endelevu.
Mkutano huo umewakutanisha viongozi wa sekta ya maji kutoka mikoa mbalimbali ili kujadili mikakati ya kuimarisha utendaji wa mamlaka za maji na kufanikisha lengo la kitaifa la upatikanaji wa maji kwa wote.
Ends.








0 Comments