USHIRIKIANO NDANI YA Arusha NDIO NGUZO YA MAENDELEO — MEYA AKEMEA RUSHWA, ATAKA UADILIFU KWA WATUMISHI
Na Joseph Ngilisho — ARUSHA
Meya wa Jiji la Arusha, Maxmilin Iranghe, amesisitiza mshikamano wa taasisi na wadau wa maendeleo kuwa ndiyo msingi wa ustawi wa jiji, huku akiwataka watumishi wa umma kuzingatia uadilifu na kuacha vitendo vya rushwa vinavyodhoofisha utoaji wa huduma.
Akifungua kikao cha Baraza la Madiwani wa Jiji la Arusha, Meya Iranghe alisema maendeleo endelevu ya jiji yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya mamlaka za serikali, wataalamu na wananchi, akionya kuwa migogoro ya kiutendaji huchelewesha utekelezaji wa miradi ya kimkakati.
“Serikali imetekeleza wajibu wake kwa kuimarisha miundombinu na kuweka mazingira wezeshi ya biashara. Sasa ni jukumu letu sote kufanya kazi kwa pamoja, kila mmoja katika nafasi yake, ili kuongeza uzalishaji, mapato ya jiji na ajira kwa vijana,” alisema.
Katika hotuba yake, Meya alikemea vikali vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wachache wa jiji, akisisitiza kuwa uadilifu ni nguzo ya utumishi wa umma na sharti la kuimarisha imani ya wananchi kwa taasisi za serikali za mitaa.
“Hatutaruhusu vitendo vya rushwa kuharibu juhudi za maendeleo. Tunahitaji uwajibikaji, nidhamu ya kazi na uadilifu usiotetereka ili Arusha iendelee kuwa kitovu cha uwekezaji na huduma bora kwa wananchi,” alisisitiza.
Aidha, alieleza kuwa jiji linaendelea kuvutia miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma za kijamii, kupanua wigo wa mapato ya ndani na kuunda ajira endelevu, akitoa wito kwa wadau wote kuunga mkono jitihada hizo kwa mshikamano na uwazi.




Post a Comment