DC MKUDE ASISITIZA UADILIFU NA USIMAMIZI THABITI WA MAPATO—BARAZA LA MADIWANI Arusha LALENGA KUJIENDESHA KWA MAPATO YA NDANI
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amewataka madiwani wa Jiji la Arusha kuongoza kwa hekima, utii na nidhamu, akisisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa mapato na uadilifu katika utumishi wa umma ndiyo msingi wa maendeleo ya jiji hilo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha pili cha robo mwaka cha Baraza la Madiwani, Mkude alisema mafanikio ya Arusha yatategemea dhamira ya viongozi katika kutatua changamoto za wananchi na kusimamia kikamilifu vyanzo vya mapato vilivyopo.
“Tuongoze kwa upendo na kufuata kanuni na taratibu. Rais amesisitiza ukusanyaji wa mapato, na ni wajibu wetu kuhakikisha vyanzo vyote vinakusanywa ipasavyo bila upotevu,” alisema Mkude, akionya kuwa baadhi ya vyanzo bado havifikii kiwango cha makusanyo kinachotarajiwa.
Katika kikao hicho, Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranghe, alitangaza kuwa Baraza la Madiwani limejipanga kulifanya jiji hilo kuwa la kwanza nchini kujiendesha kwa mapato ya ndani bila kutegemea ruzuku kutoka Serikali Kuu.
Iranghe alisema jiji lina uwezo wa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 150 kwa mwaka huku bajeti ya matumizi ikiwa takribani bilioni 130, hali inayotarajiwa kulizalishia ziada ya bilioni 20.
“Ziada hiyo tutairudisha Serikalini kusaidia halmashauri za pembezoni. Hii ni hatua ya kujenga mfumo imara wa kujitegemea kiuchumi,” alisema.
Alieleza kuwa ongezeko la mapato litatokana na kuboresha machinjio ya Sakina, kuendeleza miradi ya hoteli za kitalii, kuimarisha miundombinu ya barabara, pamoja na ubia na sekta binafsi katika ujenzi wa majengo ya biashara na stendi za kisasa.
Aidha, aliwataka madiwani kuhamasisha wananchi kuchangamkia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na jiji, huku akiiagiza Idara ya Maendeleo ya Jamii kusimamia kwa karibu marejesho ya mikopo hiyo.
Baraza hilo lilihitimishwa kwa wito wa viongozi kushirikiana kwa karibu na wananchi katika kusimamia maendeleo, huku Mkude akisisitiza kuwa mafanikio ya Arusha yanategemea uwajibikaji wa kila kiongozi katika nafasi yake.
“Maendeleo ya jiji letu yapo mikononi mwetu. Tukisimamia mapato, tukaheshimu sheria na kuwahudumia wananchi kwa moyo mmoja, Arusha itakuwa mfano wa kuigwa nchini,” alisisitiza.
.................Ends...........









0 Comments