KATAPILA LA JIJI LA Arusha LA LALA ZAIDI YA MIEZI SITA, DIWANI AIBUA HOJA NZITO BARAZANI
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
Diwani wa Kata ya Olasiti, Alex Martin, ameibua hoja nzito katika kikao cha Baraza la Madiwani la Jiji la Arusha akitaka maelezo ya kina kuhusu kutofanya kazi kwa zaidi ya miezi sita kwa katapila jipya la kuchonga barabara, lililonunuliwa takribani mwaka mmoja uliopita.
Akiuliza swali la papo kwa papo leo februali 13,2026 katika kikao cha pili cha robo ya Mwaka, diwani huyo alieleza kushangazwa na kusimama kwa nyenzo hiyo muhimu ya ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa madai ya kuisha kwa matairi, hali iliyosababisha mtambo huo kusimama bila kutoa huduma kwa wananchi katika kata mbalimbali za jiji hilo.
Alisema kuwa wakati wa mapokezi ya katapila hilo, halmashauri ilifanya hafla kubwa iliyoambatana na matarajio makubwa ya wananchi kuhusu uboreshaji wa barabara, lakini matumaini hayo yamefifia kutokana na kusuasua kwa matengenezo madogo yanayohitajika ili kulirejesha kazini.
Hafla nzito ya uzinduzi wa mitambo mipya ya jiji January 28,2025
“Ni jambo la kusikitisha na la aibu kwa halmashauri ya jiji linaloendelea kukua kwa kasi ya mapato kushindwa kununua matairi kwa zaidi ya miezi sita, huku wananchi wakisubiri huduma za barabara,” alisema Alex Martin alipozungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa baraza.
Alisisitiza kuwa kuchelewa huko kunadhoofisha ufanisi wa uwekezaji wa umma na kuchelewesha jitihada za kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo yanayokua kwa kasi ndani ya jiji.
Akijibu hoja hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dkt Nindwa Maduhu, aliliambia baraza kuwa ununuzi wa matairi mapya kwa katapila hilo pamoja na magari mengine ya jiji unahitaji takribani shilingi milioni 52.
“Mhe. Mwenyekiti, kwa mujibu wa taarifa niliyonayo kufikia leo tarehe 13, hatua za mwisho za mkataba wa usambazaji wa matairi hayo zinaendelea kukamilishwa. Baada ya kusainiwa, usambazaji utachukua kati ya siku saba hadi 14, lakini kutokana na umuhimu wake tutahakikisha yanawasilishwa kwa wakati pamoja na vipuri vingine vinavyohitajika ili mtambo huo urejee kazini kabla ya msimu wa mvua kuanza,” alisema Dkt Maduhu.
Aliongeza kuwa uongozi wa jiji unatambua umuhimu wa mtambo huo katika kazi za uchongaji na matengenezo ya barabara, na umejipanga kuhakikisha unarejea kazini haraka ili kuimarisha miundombinu ya usafiri na huduma kwa wananchi.
Hoja hiyo imeibua mjadala mpana miongoni mwa madiwani kuhusu usimamizi wa rasilimali za umma na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika jiji la Arusha linaloendelea kukua kwa kasi ya shughuli za kiuchumi na idadi ya watu.
Ends








0 Comments