TAMASHA LA MAONESHO YA UTAMADUNI NA MILA ST.l AUGUSTINE ARUSHA LAFANA,JIJI LA ARUSHA LAAHIDI USHIRIKIANO

Na Joseph Ngilisho — Arusha


Arusha — Jiji la Arusha limeahidi kuendeleza na kuimarisha maonesho ya utalii wa kitamaduni yanayofanyika katika Chuo Kikuu cha St. Augustine Tanzania (SAUT) tawi la Arusha, likitaja utamaduni kuwa rasilimali muhimu ya uchumi wa utalii na utambulisho wa taifa.


Ahadi hiyo ilitolewa leo February 13,2026 na Afisa Utamaduni wa Jiji la Arusha, Benson Maneno, alipokuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Maonesho ya Tamaduni na Mila za Kitanzania lililowakutanisha wanafunzi wa chuo hicho pamoja na wageni kutoka vyuo mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Arusha.

Katika tamasha hilo, takribani makabila 10 yaliwasilisha ngoma za asili, vyakula vya jadi na mavazi ya kitamaduni kwa lengo la kukuza utalii wa utamaduni, kutangaza taasisi za elimu na kuongeza uelewa wa vijana kuhusu asili na urithi wa jamii za Tanzania.

Mbali na wanafunzi wa SAUT, tukio hilo lilihudhuriwa na wageni kutoka vyuo vikuu mbalimbali vya Arusha na mikoa mingine, wakiwemo washiriki kutoka Zanzibar pamoja na wawakilishi wa taasisi zinazohusiana na sekta ya utalii, hatua iliyoongeza hadhi ya tamasha hilo kuwa jukwaa la kitaifa la sanaa na urithi wa jamii.


Akizungumza katika hafla hiyo, Maneno alisema maonesho hayo ni darasa hai la kuhifadhi na kurithisha mila na desturi kwa vizazi vipya huku yakitoa fursa kwa vijana kujifunza kwa vitendo sanaa za jadi na thamani ya utambulisho wa taifa.

“Arusha ni kitovu cha utalii nchini, na utamaduni ni sehemu hai ya uchumi wake. Tunataka vijana waone fursa zilizopo katika sanaa na utamaduni na jinsi zinavyoweza kuchangia maendeleo yao binafsi na ya taifa,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa SAUT Arusha, Fr. Charles Rufyiriza, alisisitiza kuwa utamaduni ni lango la msingi la sekta ya utalii kwa kuwa mtalii hukutana kwanza na maisha halisi ya jamii kabla ya vivutio vingine.

“Utamaduni unamkaribisha mgeni kabla hata ya kuona vivutio vya kiasili. Lugha, chakula, mavazi na desturi za wenyeji ndizo hatua ya kwanza ya safari ya utalii,” alisema.

Aliongeza kuwa tamasha hilo limebuniwa mahsusi kuwapa wanafunzi wa idara ya utalii na ukarimu fursa ya kujifunza kwa vitendo, huku pia likikuza mshikamano wa kitaifa kwa kuwaunganisha vijana kutoka tamaduni mbalimbali chini ya lengo la pamoja la maendeleo ya taifa.

Katika risala yao iliyosomwa na mwanafunzi Ibaya Titus, wanafunzi wa SAUT waliitaka jamii kuendeleza na kulinda utamaduni wa Kitanzania wakieleza kuwa ni urithi unaobeba historia, maadili na utambulisho wa taifa. 

Walitaja changamoto zinazoikabili sekta hiyo kuwa ni kupotea kwa baadhi ya mila kutokana na mabadiliko ya kijamii, mwamko mdogo wa vijana na ufinyu wa rasilimali za kuhifadhi urithi wa taifa.

Aidha, walipendekeza kuongezwa kwa uwekezaji katika miradi ya utamaduni, kuanzishwa kwa vazi rasmi la taifa na kuimarishwa kwa matumizi ya teknolojia katika kuhifadhi na kusambaza urithi wa kitamaduni ndani na nje ya nchi.

Halmashauri ya Jiji la Arusha imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na taasisi za elimu, wadau wa sanaa na sekta ya utalii kuhakikisha maonesho hayo yanafanyika kila mwaka kwa ubora zaidi, sambamba na kuimarisha mazingira rafiki kwa shughuli za kitamaduni.

Tamasha hilo limeunganisha elimu, sanaa na uchumi, likitoa taswira ya utamaduni kama nyenzo ya maendeleo endelevu na kuimarisha nafasi ya Arusha kama lango la utalii wa kitamaduni nchini.

Kwa upande wake mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) tawi la Arusha, Subiraga Brighton Masebo, alisema kuwa ubunifu katika ufundishaji wa masomo ya utamaduni umezaa Tamasha la Sauti Massive Cultural Festival linalowapa wanafunzi nafasi ya kujifunza kwa vitendo.

Akizungumza wakati wa tamasha hilo chuoni hapo, Masebo alisema anafundisha kozi ya Cross-Cultural Management inayolenga kuwajengea wanafunzi uelewa wa tamaduni mbalimbali kupitia nadharia na vitendo.

Alifafanua kuwa alianzisha mbinu ya kuwagawa wanafunzi katika makundi ya kikabila ili kila kundi liwasilishe utamaduni wake kupitia mavazi ya asili, vyakula vya jadi, ngoma na mila nyingine zinazowatambulisha.

“Utamaduni hauwezi kufahamika kwa kusoma pekee. Lazima uonyeshwe kwa vitendo ili wanafunzi wauelewe kwa kina,” alisema Masebo.

Alieleza kuwa mwanzoni shughuli hiyo ilikuwa sehemu ya tathmini ya darasani, lakini kadri miaka ilivyopita ilikua na kuvutia wadau mbalimbali wa elimu na taasisi nyingine walioanza kuhudhuria kushuhudia ubunifu huo wa kielimu.

Kwa mujibu wake, mwitikio chanya kutoka kwa wanafunzi na wageni umeifanya shughuli hiyo kuwa jukwaa la kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuthamini urithi wa kitamaduni wa Tanzania.












.........Ends.......


Post a Comment

0 Comments