Friends of Batuli Waadhimisha Valentine kwa Kuwagusa Watoto Yatima kwa Msaada na Upendo
Na Joseph Ngilisho – Arusha
Kundi la kijamii la Friends of Batuli la jijini Arusha, limeadhimisha Siku ya Wapendanao kwa tendo la huruma na mshikamano wa kijamii, baada ya kutembelea kituo cha kulea watoto yatima cha Kindness Children Care lililopo Kijenge Juu, Kata ya Kimandoro, na kukabidhi msaada wa vyakula na mahitaji ya msingi kwa watoto wanaolelewa kituoni hapo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwalimu Ali Ramadhan alisema lengo la tukio hilo halikuwa tu kutoa misaada ya mahitaji muhimu, bali pia kuwapa watoto faraja na kuwathibitishia kuwa wanathaminiwa na jamii.
“Tumekuja kuwaonyesha watoto hawa kuwa wanapendwa na ni sehemu muhimu ya jamii yetu. Upendo ni msingi wa kuwajengea matumaini na kuimarisha ndoto zao,” alisema Ramadhan.
Misaada iliyokabidhiwa ni pamoja na sabuni za kufulia na kuogea, pamoja na vyakula ikiwemo mchele, mahindi, maharage na sukari kwa matumizi ya kila siku ya watoto hao. Ramadhan alipongeza juhudi za uongozi wa kituo kwa kujitoa kuwalea watoto wenye uhitaji, akitoa wito kwa wananchi na wadau kushirikiana na taasisi za malezi ili kuimarisha ustawi wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Aidha, aliwahimiza watoto wanaopata fursa ya elimu kusoma kwa bidii ili baadaye waweze kuitumikia jamii kama wanavyosaidiwa sasa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kituo hicho, Mchungaji Yohanna Mwampamba, alieleza kuwa msaada huo umeongeza furaha na matumaini kwa watoto 63 wanaolelewa hapo, wakiwemo yatima na wenye ulemavu wanaopata huduma za malezi na elimu kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo.
“Upendo wa wadau unatupa nguvu ya kuendelea kuwalea watoto hawa kwa heshima na utu. Tunaamini mchango huu utaboresha zaidi mazingira yao ya makuzi,” alisema Mwampamba.
Alibainisha kuwa pamoja na mafanikio ya huduma za kila siku, kituo kinakabiliwa na changamoto ya kulipa gharama za pango na kinahitaji kununua kiwanja chenye thamani ya shilingi milioni 150 ili kujenga makazi ya kudumu kwa watoto.
Mwampamba alisisitiza kuwa licha ya kutopokea ufadhili kutoka nje ya nchi, Watanzania kutoka makanisani, misikitini na makundi mbalimbali wameendelea kuwa nguzo muhimu ya uendeshaji wa kituo hicho.
Naye mwakilishi wa familia ya Friends of Batuli, Glory Kaaya, alihimiza jamii kujenga utamaduni wa kusaidiana, akisema baraka za mtu hupata maana zaidi zinapogusa maisha ya wengine, hususan watoto wasiojiweza.
“Hatuhitaji kuwa na vingi ili kutoa. Hata kile kidogo tukishirikiana kwa upendo kinaweza kubadili maisha ya wengi,” alisema Kaaya.
Aliongeza kuwa kuchagua kuwasaidia wahitaji katika siku maalum kama Siku ya Wapendanao ni njia ya kueneza ujumbe wa huruma na mshikamano wa kijamii, akitoa wito kwa watu wenye uwezo wa kifedha na wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia malezi ya watoto wanaokosa huduma za msingi.
Kwa ujumla, tukio hilo limeonesha kuwa maendeleo ya jamii hayaamuliwi na rasilimali pekee, bali na moyo wa kushirikiana—ambapo hata mchango mdogo, unapounganishwa na upendo, huleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wenye uhitaji.
Ends..






















0 Comments