Programu ya Afya ya “Health IQ” Yazinduliwa Arusha, Yalenga Mapinduzi ya Tathmini ya Afya Kidijitali
Na Joseph Ngilisho – Arusha
Mradi wa kiteknolojia wa afya unaotumia akili bandia, Health IQ, umeanzishwa jijini Arusha kwa lengo la kuwasaidia wananchi na watalii kujitathmini hali zao za afya ndani ya muda mfupi kupitia simu janja.
Mwanzilishi wa mradi huo, Ahmed Raza maarufu kama Dr. Raza Junior, alisema programu hiyo hutoa tathmini ya afya kwa kuzingatia masuala ya kimwili, afya ya akili, mtindo wa maisha na hali ya kijamii, kisha kumpatia mtumiaji mwongozo wa hatua za kuchukua kuboresha afya yake.
Akizungumza na wanafunzi wa chuo kikuu cha St Augustine katika tamasha la Maonesho ya Tamaduni na Mila za Kitanzania chuoni hapo, Ahmed Raza.
Alieleza kuwa programu hiyo ni bure kupakua na kutumia kupitia majukwaa ya simu janja, ambapo mtumiaji hujibu maswali machache yanayochambuliwa na mfumo wenye uwezo wa kufikiri kwa mtindo unaofanana na daktari.
Raza alisema ubunifu huo ulitokana na uzoefu wa familia yake ya kitabibu na hamasa ya kuboresha upatikanaji wa taarifa za afya kwa urahisi bila gharama kubwa.
“Tumejenga mfumo unaomwezesha mtu kuelewa hali yake ya afya na kuanza kuchukua hatua sahihi mapema. Endapo tathmini itaonyesha hitaji la huduma ya kitabibu, mtumiaji ataelekezwa kumuona daktari,” alisema.
Kwa mujibu wake, mradi huo wenye makao makuu Arusha umeanza kupata watumiaji katika zaidi ya nchi 80 ndani ya mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake, hatua anayosema imechangiwa na ukuaji wa sekta ya utalii na ushiriki wa wanafunzi wa vyuo vya utalii nchini.
Alitaja ushirikiano na taasisi mbalimbali ikiwemo Arusha Technical College kuwa umechangia kueneza matumizi ya programu hiyo kimataifa kupitia wahitimu wanaofanya kazi katika sekta ya utalii nje ya nchi.
Raza alisisitiza kuwa afya bora ya wadau wa utalii ni muhimu katika kuimarisha taswira ya Tanzania kimataifa, akibainisha kuwa nchi ina rasilimali zaidi ya vivutio vya asili kama Mount Kilimanjaro na Mount Meru, ikiwemo ubunifu wa kiteknolojia unaoibukia.
Aliongeza kuwa kuanzishwa kwa programu hiyo Arusha ni ishara ya mchango wa vijana wa Tanzania katika maendeleo ya teknolojia duniani na fursa ya kuunganisha sekta za afya, elimu na utalii.
Ends.....



0 Comments