SERIKALI YAMUENZI EDWIN MTEI KWA VITENDO, MWIGULU ATOA MAAGIZO MAZITO

SERIKALI YAMUENZI EDWIN MTEI KWA VITENDO, MWIGULU ATOA MAAGIZO MAZITO

Na Joseph Ngilisho- ARUSHA 

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza dhamira yake ya kumuenzi aliyekuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), marehemu Edwin Mtei, kwa vitendo vinavyoakisi mchango wake mkubwa katika ujenzi wa Taifa, hususan demokrasia, haki na maendeleo ya kiuchumi.

Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, alipokuwa akitoa salamu za Serikali katika msiba wa marehemu Mtei uliofanyika nyumbani kwake, Tengeru mkoani Arusha, kwa niaba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Waziri Mkuu alisema marehemu Mtei alikuwa mmoja wa watu waliotoa mchango wa kipekee katika historia ya Tanzania, akitaja kuwa ni mwanzilishi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania, Waziri wa Fedha wa awali na mwanasiasa aliyesimamia kwa vitendo misingi ya demokrasia ya vyama vingi.

“Mheshimiwa Rais amenielekeza nije kumwakilisha na kufikisha salamu za Serikali, lakini pia amesisitiza kuwa kumuenzi Mzee Edwin Mtei hakupaswi kuwa kwa maneno tu, bali kwa vitendo,” alisema Waziri Mkuu.




Katika kuonesha heshima hiyo, Waziri Mkuu alisema Rais ameielekeza Benki Kuu ya Tanzania kushiriki kikamilifu katika shughuli za mazishi na kutoa heshima zote stahiki kwa marehemu, kama mwanzilishi na Gavana wa kwanza wa taasisi hiyo nyeti ya kifedha, sambamba na heshima zinazotolewa kwa magavana wengine wote waliowahi kulitumikia Taifa.

Aidha, Waziri Mkuu alieleza kuwa Waziri wa Fedha ameagizwa kushiriki katika msiba huo kutokana na mchango wa marehemu alipowahi kuhudumu kama Waziri wa Fedha, huku Waziri wa Elimu pia akishiriki kama mtoto wa nyumbani, akiwakilishwa na Profesa Mkenda.

MAAGIZO YA MIRADI YA MAENDELEO

Katika hatua iliyotafsiriwa kama kumbukumbu ya kudumu kwa marehemu, Waziri Mkuu alitoa maelekezo mazito ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, hususan ujenzi wa barabara ya njia nne kuanzia Tengeru hadi Usa, na kuendelea hadi Kia na Moshi.

Alisema mchakato wa manunuzi kwa kipande cha Tengeru–Usa ulikuwa umekamilika, hivyo akaelekeza ujenzi huo uanze mara moja. Kwa kipande cha Usa–Kia chenye urefu wa kilomita 28, alisema usanifu umefikia zaidi ya asilimia 80 na akaagiza Wizara ya Ujenzi na TANROADS kukamilisha haraka usanifu uliobaki na kutangaza zabuni.

“Fedha zipo. Nataka mkandarasi apatikane haraka na ujenzi uanze. Mimi mwenyewe nitasimamia utekelezaji wake,” alisema kwa msisitizo.


Akiangazia msimamo wa marehemu Mtei kuhusu haki, Waziri Mkuu aligusia mgogoro wa shamba la Mlinga Estate, akieleza kuwa kulikuwa na makubaliano ya wananchi kunufaika na maeneo yao, lakini mchakato huo uliingia dosari kutokana na mabadiliko yasiyo halali ya umiliki.

Aliagiza ndani ya mwezi mmoja, marekebisho yote yafanyike, huku Mkoa na Kamishna wa Ardhi wakisimamia kwa karibu kuhakikisha wananchi wanaostahili wanapewa maeneo yao kwa mujibu wa makubaliano ya awali.

Katika kuenzi mapenzi ya marehemu kwa maendeleo ya wananchi wa kawaida, Waziri Mkuu aliagiza mikoa, halmashauri na wakurugenzi wote kubaini maeneo yanayofanyika biashara ndogondogo na kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha mazingira ya wafanyabiashara.

Alisisitiza kujengwa kwa miundombinu stahiki ikiwemo mapaa, sakafu na nguzo imara, ili wafanyabiashara wafanye shughuli zao katika mazingira salama na yenye heshima, tofauti na hali ya sasa inayosababisha adha wakati wa mvua.

Waziri Mkuu alihitimisha kwa kusema kuwa marehemu Edwin Mtei ataendelea kukumbukwa kama kiongozi mwenye ujasiri, maono na uzalendo wa dhati, aliyependa maendeleo na kusimamia haki bila kuyumba.

“Haya tunayoyatekeleza ni alama ya heshima na kumbukumbu ya kudumu ya maisha na mchango mkubwa wa Mzee wetu Edwin Mtei kwa Taifa la Tanzania,” alisema.

Ends .

Post a Comment

0 Comments