MEYA ARUSHA AZINDUA AWAMU YA TATU YA ‘NG’ARISHA JIJI’, ATOA MSISITIZO USIMAMIZI NA ELIMU YA MAZINGIRA
Na Joseph Ngilisho – ArushaDigital
Katika kuendeleza jitihada za kulinda afya ya wananchi na kuboresha mandhari ya Jiji la Arusha, Mstahiki Meya wa Jiji hilo, Mhe. Maxmillian Matle Iranqhe, leo Januari 24, 2026, amezindua rasmi awamu ya tatu ya kampeni ya usafi wa mazingira ijulikanayo kama ‘Ng’arisha Jiji’, uzinduzi uliofanyika katika Kata ya Daraja II.
Uzinduzi wa kampeni hiyo uliambatana na zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika katika eneo la Kituo cha Afya Daraja II, ambapo wananchi, viongozi wa serikali za mitaa, watendaji wa kata pamoja na maafisa afya walishiriki kwa pamoja, hali iliyoonesha dhamira ya uongozi wa jiji kushirikiana na jamii katika kulinda mazingira na afya ya umma.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kushiriki zoezi hilo, Mhe. Iranqhe alieleza kuwa kampeni ya ‘Ng’arisha Jiji’ inalenga kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu usafi wa mazingira, kutoka kufanya usafi kwa mazoea ya msimu au siku maalum, kwenda kwenye utamaduni endelevu wa uwajibikaji wa kila siku.
Alielekeza Watendaji wa Kata kuhakikisha wanasimamia kikamilifu majukumu ya Maafisa Afya katika maeneo yao, akisisitiza kuwa usafi wa mazingira ni jukumu la kudumu linalohitaji ufuatiliaji wa karibu, mipango madhubuti na tathmini ya mara kwa mara.
“Usafi wa mazingira haupaswi kuwa zoezi la kusubiri Jumamosi au kampeni maalum pekee. Ni lazima uwe sehemu ya maisha ya kila siku ya wananchi wetu, kwani mazingira machafu ni chanzo kikubwa cha magonjwa yanayoweza kuzuilika,” alisema Meya huyo.
Aidha, Mhe. Iranqhe alisisitiza umuhimu wa utoaji wa elimu ya mara kwa mara kwa wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira, akibainisha kuwa mabadiliko ya kweli ya usafi hayawezi kupatikana bila wananchi kuelewa wajibu wao binafsi na athari za moja kwa moja za uchafu kwa afya zao na uchumi wa jiji.
Aliwahimiza wakazi wa Jiji la Arusha kuhakikisha usafi katika maeneo yao ya makazi, maeneo ya wazi pamoja na maeneo ya biashara, akieleza kuwa wafanyabiashara wanapaswa kufanya usafi kabla ya kufungua shughuli zao asubuhi na baada ya kufunga jioni, kama sehemu ya nidhamu ya kazi na ulinzi wa afya ya wateja wao.
Kwa mujibu wa Meya huyo, utekelezaji thabiti wa kampeni ya ‘Ng’arisha Jiji’ utasaidia kupunguza magonjwa ya mlipuko yanayotokana na mazingira machafu, kuboresha taswira ya Jiji la Arusha kama kitovu cha utalii na biashara, pamoja na kuongeza ustawi wa kijamii na kiuchumi kwa wakazi wake.
Kampeni ya ‘Ng’arisha Jiji’, ambayo sasa imeingia awamu ya tatu, inaendelea kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika Jiji la Arusha, ikilenga kujenga utamaduni wa usafi wa mazingira kama jukumu la kila mmoja, huku uongozi wa jiji ukisisitiza kuwa mafanikio ya kampeni hiyo yatategemea kwa kiasi kikubwa ushiriki wa wananchi, usimamizi madhubuti wa viongozi wa maeneo husika na uwajibikaji wa taasisi zote zinazohusika na masuala ya afya na mazingira.




0 Comments