Mbowe: Taifa Litangulize Maridhiano na Ujenzi wa Nchi Kuliko Migawanyiko ya Kisiasa
Na Joseph Ngilisho-ARUMERU
MWENYEKITI mstaafu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kuwa changamoto zinazolikabili taifa la Tanzania haziwezi kutatuliwa kwa misingi ya vyama vya siasa bali kwa kuweka mbele maslahi mapana ya nchi na mshikamano wa kitaifa.
Akizungumza leo januari 24,2026 wakati wa kutoa sala katika ibada ya maziko ya aliyekuwa kiongozi na mwasisi wa CHADEMA, Marehemu Edwin Mtei, iliyofanyika nyumbani kwa marehemu, Mbowe alisema kuwa viongozi wa kisiasa hawapaswi kutazamwa kama wachochezi au wakorofi, bali kama wadau muhimu katika ujenzi wa taifa.
Mbowe alisisitiza kuwa viongozi wa upinzani ni sehemu ya uongozi wa nchi na wanastahili kuheshimiwa kama viongozi wengine wa kitaifa, akieleza kuwa hata viongozi wakuu wa serikali wamewahi kuwatambua na kuwaheshimu katika nyakati tofauti.
“Leo si siku ya kuzungumzia vyama vya siasa, bali ni siku ya kuzungumzia nchi yetu. Tunapozungumzia maridhiano, tunazungumzia mustakabali wa Tanzania,” alisema Mbowe.
Katika kauli yake, Mbowe alitumia fursa hiyo kupeleka salamu za taifa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Watanzania wote, akibainisha kuwa CHADEMA iko tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kujenga taifa endapo kutakuwepo dhamira ya kweli kutoka upande wa serikali.
Alifafanua kuwa juhudi na msimamo wa CHADEMA si kwa ajili ya ubinafsi wa madaraka, bali ni kwa lengo la kujenga nchi inayotambua makundi yote ya wananchi na kutoa haki na fursa sawa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.
Mbowe alikumbusha historia ya taifa, akisema Tanzania imewahi kujenga misingi ya demokrasia ya vyama vingi, kuwa na Bunge la vyama vingi na kiongozi wa upinzani aliyedumu kwa zaidi ya miaka kumi, jambo lililothibitisha uwezekano wa kuishi kwa misingi ya kisiasa yenye kuheshimiana.
Akihitimisha kauli yake, Mbowe aliwataka viongozi wa CHADEMA na Watanzania kwa ujumla kuendelea kutafuta suluhu ya kitaifa kupitia njia za amani na kisheria, huku akisisitiza kuwa mchakato huo utakuwa na maana endapo haki za kikatiba zitaheshimiwa.
“CHADEMA ifanye kazi zake kama Katiba inavyoruhusu. Wanaodai haki zao wapewe haki zao. Waliokamatwa au kushtakiwa kwa sababu za kisiasa kwa kesi za kugumaguma waachiliwe kwa kufuata misingi ya haki,” alisema.
Ibada ya maziko ya Marehemu Edwin Mtei ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kisiasa, wa dini na wananchi, waliokuja kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo aliyetoa mchango mkubwa katika historia ya siasa za vyama vingi nchini Tanzania.
Ends..


0 Comments